
MWANAMUZIKI wa muziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’
amekuja na mashindano ya mpira kila mkoa yatakayoitwa Bingwa la Mtaa ambayo yatawahusisha madereva wa bodaboda na bajaji.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Diamond amesema ameamua kuja na mashindano hayo kama sehemu ya kurudisha kwa jamii, kuwaleta pamoja madereva hao na yataibua fursa ya kupata vipaji vipya.
Amesema wamepeleka mashindano hayo kwa watu ambao wamekuwa wakisapoti muziki wao.
Diamond amesema washindi katika mashindano hayo kwa mikoani wa kwanza atapata Sh milioni 5, wa pili Sh milioni 3 na watatu Sh milioni 2 na kwa upande wa Mkoa wa Dar es
Salaam mshindi wa kwanza atapata Sh milioni 10, wa pili Sh milioni 5 na wa tatu Sh milioni 3.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa waendesha bodaboda na bajaji Mkoa wa Dar es Salaam, Maiko Masawe, amesema wamepokea jambo hilo kwa mikono miwili na kuahidi kutoa ushirikiano.
Amesema kitendo hicho kimewafanya kujiona wenye thamani mbele ya jamii na
kubainisha kuwa fedha watakazozipata zitawasaidia katika shughuli zao.
Mkoa utakaofungua dimba kwa mashindano hayo ni Mbeya ukifuatiwa na Morogoro na kote huko siku ya fainali mchezo utakoisha kutashushwa burudani ya muziki kutoka kwa wasanii
wa lebo ya WCB.
Kwa upande wake msanii Zuhura Othman ‘Zuchu’ amesema yeye kama mmoja wa mabalozi wa Wasafi anaomba udhamini kama huo uende pia kwenye Ndondo Cup ya Zanzibar ili na wao wanufaike.