Ligi Daraja La Kwanza

Dar City yatinga fainali ya ligi ya mkoa

DAR ES SALAAM: DAR CITY imefuzu fainali ya Ligi ya Kikapu mkoa wa Dar es Salaam baada ya kuifunga Vijana kwa pointi 65-40 katika mchezo wa tatu wa nusu fainali na kufikisha ushindi wa michezo mitatu mfululizo.

Mabingwa hao watetezi walianza mfululizo huo kwa ushindi wa pointi 61-56 kabla ya kuendeleza ubabe katika mchezo wa pili, wakishinda kwa tofauti kubwa ya pointi 84-31 na hivyo kuhitaji ushindi mmoja pekee katika michezo mitatu iliyosalia ili kufuzu.

Ushindi wa jana wa pointi 65-40 ulihitimisha mfululizo huo kwa Dar City bila kupoteza mchezo, na sasa timu hiyo inaendelea na maandalizi ya fainali katika harakati za kutetea ubingwa wake.

Kwa mfumo wa michezo mitano unaotumika katika hatua ya nusu fainali, timu inayofikisha ushindi wa michezo mitatu ndiyo inayofuzu fainali, huku Vijana ikishindwa kupata ushindi katika michezo yote mitatu.

Dar City sasa itasubiri mshindi kati ya Stein Warriors na Pazi ambao bado wanaendelea na mfululizo wao wa nusu fainali. Stein Warriors tayari imepata ushindi katika michezo miwili na inahitaji ushindi mmoja zaidi kufuzu fainali.

Related Articles

Back to top button