Collins Saliboko kugombea uongozi kimataifa

DAR ES SALAAM: MCHEZAJI wa timu ya Taifa ya kuogelea Collins Saliboko ameteuliwa kuwania nafasi ya uongozi katika Kamati ya Waogeleaji ya Shirikisho la Kimataifa la Kuogelea na Michezo ya Maji.
Kwa mujibu wa taarifa ya Chama cha Kuogelea Tanzania TSA iliyotolewa na Msemaji wao Sebastian Kolowa, hii ni hatua ya kihistoria kwa Tanzania, kwani ni mara ya kwanza kwa Mtanzania kuwania nafasi hii ya heshima ya kimataifa.
Aidha, Collins ndiye muogeleaji pekee kutoka Afrika Mashariki aliyechaguliwa kushiriki katika mchakato huu muhimu wa uongozi.
“Chama cha Kuogelea Tanzania kinayo furaha kubwa kutangaza kuwa muogeleaji wetu mahiri, Collins Saliboko, ameteuliwa kuwania nafasi ya uongozi katika Kamati ya Waogeleaji ya Shirikisho la Kimataifa la Kuogelea na Michezo ya Maji World Aquatics,
“Tuna kila sababu ya kumpongeza kwa dhati kwa hatua hii kubwa na ya kipekee,” amesema .
Chama hicho kimeomba jamii ya waogeleaji na watanzania kwa ujumla waendelee kumuombea na kumuunga mkono Collins ili afanikishe ndoto hii na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania kimataifa.