Ligi Kuu

Christina Mwagala azitumia Salamu Simba, Yanga

ARUSHA: OFISA Habari wa TRA, Christina Mwagala, amezitumia salamu klabu za Simba na Yanga akisisitiza kuwa ni vyema zikawa tayari kucheza michezo yao ya Ligi Kuu katika viwanja vya mikoani badala ya kuonekana kama hazitaki kusafiri nje ya Dar es Salaam.

Mwagala amesema TRA imechagua Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha kuwa uwanja wake wa nyumbani na kwamba timu zitakazokwenda kucheza huko zinapaswa kuwa tayari kwa mazingira hayo kama ilivyo kwa timu nyingine zinazocheza mikoani.

“Sisi TRA tumechagua Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kuwa uwanja wetu wa nyumbani, kwa hiyo nazitaka zile timu ambazo zinaonekana kama hazitaki kucheza mikoani wajue kwamba hata wao hawana viwanja vyao binafsi. Lazima tuzoee kucheza popote pale ambapo mechi imepangwa,” Amesema Mwagala.

Kauli hiyo ya Mwagala inakuja siku moja baada ya Yanga kukumbwa na sintofahamu ya uwanja katika mchezo wake wa Ligi Kuu dhidi ya Tanzania Prisons, ambao awali ulipangwa kuchezwa Tabora kabla ya taarifa za baadaye kueleza uwezekano wa kuhamishiwa Dodoma.

Wakati huo huo, TRA inaendelea na maandalizi ya kuikaribisha Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaotarajiwa kuchezwa Machi 14 mwaka huu katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Mwagala amesema timu yao imejipanga kuhakikisha inafanya vizuri katika mchezo huo muhimu, huku akiwakaribisha mashabiki wa soka Arusha na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yao.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button