Masumbwi

Changarawe, Macho wang’ara Kenya

NAIROBI: MABONDIA wa timu ya Taifa ya ngumi ya Tanzania, Yusuph Changarawe na Zulfa Macho wamefuzu hatua ya fainali ya mashindano ya ngumi barani Afrika yanayofanyika nchini Kenya.

Changarawe amefuzu hatua ya hiyo baada ya kumtandika kwa ‘points’ bondia Fotouo Totap raia wa Cameroon.

Nahodha wa timu ya Taifa ya ngumi ya Tanzania kwa upande wa wanawake bondia Zulfa Macho naye ametinga hatua hiyo ya juu baada ya kumpiga kwa kishindo Deborah Bawo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DR Congo) kwa pointi 5-0 katika pambano la nusu fainali lililochezwa jana jijini Nairobi.

Ushindi huu ni wa kisasi kwa Zulfa, ambaye mwaka 2024 alipoteza kwa pointi 3-2 dhidi ya mpinzani huyo katika Mashindano ya Afrika yaliyofanyika Kinshasa, DR Congo.

Zulfa sasa atacheza fainali siku ya Ijumaa, akimenyana na Amina Martha kutoka Kenya A, bondia wa kwanza wa kike wa Kenya kushinda medali kwenye Mashindano ya Mataifa ya Afrika (African Games) yaliyofanyika Accra, Ghana 2024.

Mashindano hayo ambayo yanafanyika katika uwanja wa ndani wa Kasarani uliopo jijini Nairobi yatafikia tamati kesho Ijumaa ya Oktoba 24 mwaka huu ambapo ndipo mapambano ya fainali yatafanyika.

Related Articles

Back to top button