Nyumbani

Chama, Mayele kuvunja rekodi zao?

CLATOUS Chama mwamba wa Lusaka Zambia ni kiungo sahihi na tegemeo kwenye kikosi cha Simba.

Kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama.

Tangu kujiunga na wekundu hao mwaka juzi bado hajachuja bali anazidi kuwa bora. Hata kama akishuka ni kidogo tu na akisemwa hujirekebisha na kurudi kwenye ubora.

Unaweza kusema Chama ndiye kiungo bora pale Simba na hata kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na kile anachokifanya siku hadi siku na kuisaidia timu yake kupata matokeo mazuri katika muda sahihi.

Mchezaji huyo ni mnyumbulikaji na anajua chenga, zile visigino ndo zake, amekuwa akichangia pasi nyingi za mabao lakini pia, ni mchezaji asiyekamatika kiurahisi kwani amekuwa akisumbua ngome nyingi za ulinzi kwa timu pinzani.

Takwimu za misimu mitatu zinaonesha namna gani mchezaji huyo alistahili zile tuzo tatu
alizopata msimu wa 2019/2020 za wachezaji bora. Chama kipindi kile alipata tuzo tatu kwa maana ya mchezaji bora, kiungo bora na kikosi bora cha msimu.

Msimu wa mwaka juzi alifunga mabao mawili na kuchangia pasi 10 za mabao. Alistahili tuzo kwa sababu sio tu mchango wake ulionekana kwenye ligi bali katika michuano ya kimataifa alitumia uzoefu wake kuisaidia Simba kwenye hatua mbalimbali.

Msimu wa 2020/2021 amehusika kwenye mabao 23 akifunga nane na pasi 15 za mabao kati ya 78 iliyofungwa na timu yake iliyotwaa ubingwa wakati ule.

Mchezaji huyu kama sio kuondoka na kwenda kujiunga na RS Berkane ya Morocco pengine angeibuka tena mchezaji bora na kiungo bora lakini kutokuwepo kwake tuzo ilienda kwa Feisal Salum.

Lakini mwamba amerudi tena Ligi Kuu na bado amedhihirisha yeye ni mchezaji bora baada ya kuchangia pasi 10 za mabao katika michezo 18 ya Ligi Kuu msimu huu.

Chama asipokuwepo kwenye kikosi cha wekundu pengo linaonekana wazi lakini akiwepo husumbua sana ngome za wapinzani kama sio kufunga basi huwatengenezea wenzake pasi za mabao.

Kwa mwenendo wake jinsi ulivyo, kila timu imebakiza michezo 12 hivyo, bado ana nafasi
kubwa ya kuifikia rekodi yake ya msimu wa 2021 na pengine kuivunja na kuweka rekodi mpya nyingine.

Hilo linawezekana kama ataendelea kuwa katika kiwango bora na bila kupata majeraha.
Simba mpaka sasa imefunga jumla ya mabao 40 na yeye amehusika kwenye mabao 10 ana mabao aliyofunga japo ni machache.

Kwa takwimu zake hizo inadhihirisha wazi mchezaji huyo ni hatari kwa wapinzani na kama
asipochungwa anaweza kusababisha madhara zaidi.

Wachezaji wengine wenye pasi nyingi ni Ayoub Lyanga wa Azam FC ambaye amehusika kwenye mabao saba, Saido Ntibazonkiza wa Simba aliyechangia pasi sita akiwa na timu yake ya Geita kabla ya kujiunga na wekundu hao hivi karibuni.

Sixtus Sabilo wa Mbeya City amekuwa ni mchezaji mzuri akichangia pasi sita sawa na beki
bora wa Simba Mohamed Hussein, Ally Ramadhan wa Kagera Sugar akiwa na pasi nne
za mabao sawa na Nicolaus Gyan wa Singida Big Stars.

MAYELE
Fiston Mayele unaweza kusema ndiye mshambuliaji bora mpaka sasa akiongoza kwa kufunga mabao 14 katika michezo 18. Msimu wake wa kwanza kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara ni mwaka jana akitokea klabu ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
(DRC) ambapo alifunga mabao 16.

Ilibaki kidogo tu achukue kiatu cha dhahabu cha Ligi Kuu lakini alizidiwa kidogo na
mshambuliaji wa Geita George Mpole aliyefunga mabao 17 ambaye msimu huu hakuanza
vizuri na timu yake na sasa ametimkia DRC katika timu ya FC Lupopo.

Kwa mwenendo wake wa msimu huu inaonesha kwamba Mayele anaweza kuivunja rekodi yake kwani kasi yake ya sasa ya ufungaji mabao inatisha. Anahitaji kufunga mawili tu kufikia rekodi yake ya msimu uliopita jambo ambalo linawezakana ikiwa ataendelea kupewa
ushirikiano na wenzake.

Mayele ni mshambuliaji mwenye uchu wakati wote wa kufunga, namna anavyocheza huwa akipata nafasi katika eneo sahihi halazi damu. Unaweza kusema ndiye mchezaji tegemeo
kwenye kikosi hicho cha mitaa ya Twiga na Jangwani Kariakoo.

Ni mchezaji mwenye kasi na anapokuwa eneo la hatari anajua namna ya kuwapindua mabeki wa timu pinzani hadi kufunga. Kiufupi ni mchezaji anayestahili kuitwa mshambuliaji kwa kuwa anajua kushambulia lango pale anapopata nafasi.

Bado mchezaji huyo ni kama yuko kwenye vita kwa sababu anakimbizana na mshambuliaji wa Simba, Moses Phiri ambaye naye alianza ligi kwa kasi ya hatari na mpaka sasa  mefunga mabao 10.

Bahati mbaya mchezaji huyu  kwa sasa anakabiliwa na majeraha baada ya kuumia katika
mchezo dhidi ya Kagera Sugar hivyo, anaweza kukaa nje kwa wiki mbili kutibu majeraha yake.

Hilo linaweza kumpa nafasi ya Mayele kuibuka mfalme kama atafunga kila mchezo ulioko mbele yake.

Ukiacha wachezaji hao, bado kuna wengine wanaokuja ingawa ni kwa kusuasua lakini hawapaswi kubezwa kwani wapo kwenye mbio za kuwania kiatu ambao ni Idris Mbombo wa Azam FC amefunga mabao saba sawa na Sixtus Sabilo wa Mbeya City.

Feisal Salum wa Yanga, John Bocco wa Simba na Reliants Lusajo wa Namungo kila mmoja
ana mabao sita. Bocco amecheza mechi chache na amefikisha idadi hiyo hivyo, anaweza kuwa hatari na pengine kumkimbiza Mayele kama atapata nafasi zaidi na kufunga mabao.

Related Articles

Back to top button