
KOCHA Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze amesema timu hiyo ipo tayari kwa mchezo wa 49 bila kufungwa itakapoivaa Mbeya City Novemba 26 katika mfululizo wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara.
Akizungumza na SpotiLeo Kaze amesema anaamini Yanga itapata matokeo mazuri katika mchezo huo utakaofanyika uwanja wa Benjamin Mkapa ingawa utakuwa mgumu kutokana upinzani wa Mbeya City.
Kaze amesema kurejea kwa kiungo mshambuliaji Stephane Aziz Ki na kipa Djigui Diara kutachagiza kupata ushindi katika mchezo huo.
“Aziz Ki na Diarra ni miongoni mwa wachezaji watakaocheza kwenye mechi yetu ya kesho dhidi ya Mbeya City. Uwepo wao ni msaada mkubwa kwetu katika malengo yetu ya kuchukua pointi tatu,” amesema Kaze.
Yanga ni vinara wa ligi hiyo kwa sasa wakikusanya pointi 29 katika michezo 11 huku wakiwa na rekodi ya kuwa timu pekee ambayo haijapoteza mchezo tangu msimu huu kuanza.