Canadi afuata nyayo za Damaro

SINGIDA: KIUNGO mshambuliaji wa Singida Black Stars, Marcelo Canadi ametangaza kuvunja mkataba wake na klabu hiyo.
Hilo limejiri ikiwa ni siku moja imepita tangu kiungo mwingine wa Singida, Mohamed Damaro naye kutangaza kufanya hivyo.
Canadi, raia wa Austria kupitia ujumbe aliouweka kwenye Mtandao wa Instagram, amesema amechukua uamuzi huo baada ya majadiliano na uongozi wa klabu hiyo.
Amebainisha kuwa miongoni mwa mambo mengine yaliyomwondoa ni mambo kwenda tofauti na vile alivyotarajia.
“Wakati mwingine katika mpira wa miguu, mambo huwa hayaendi kama tunavyotegemea. Baada ya mazungumzo na klabu, nimeamua kwamba muda wangu hapa umefikia mwisho. Asante Tanzania kwa kuwa na mimi. Tutaonana tena siku moja,” aliandika Canadi.
Mchezaji huyo amedumu Singida kwa miezi minne baada ya kusajiliwa Julai, mwaka huu.
Cabadi anaondoka Singida akiwa ameifungua bao moja kwenye Ligi Kuu Bara, alilofunga dhidi ya Namungo walipoibuka na ushindi wa mabao 3-2.
Mpaka sasa Singida haijasema chochote kuhusiana na hilo na SpotiLeo ilipomtafuta Ofisa Habari wa Singida, Hussein Masanza kutoa ufafanuzi, simu yake iliita bila kupokelewa.




