Bruno Fernandez: Hatushindi mechi kulinda kibarua cha mtu

MANCHESTER: NAHODHA wa Manchester United, Bruno Fernandes, amejitokeza kumuunga mkono kocha mkuu, Michael Carrick, lakini akasisitiza kuwa wachezaji hawakuhitaji kuokoa kibarua chake katika ushindi wao wa 3-2 dhidi ya AS Roma.
United ikiwa Uwanja wa Old Trafford, ilijidadavua jana Jumanne, ikitoka nyuma na kupata ushindi wa mabao 3-2, ukiwa ni ushindi wa kwanza katika mechi 10 zilizopita.
United na Carrick walionekana wameshindwa kabisa ndani ya dakika 18 za mwanzo, huku timu hiyo ya Italia ikiongoza kwa mabao mawili mapema katika mchezo huo.
Ari iliyoonyeshwa katika mchezo huo ilionyesha kulikuwa na aina fulani ya uungwaji mkono uwanjani kwa Carrick, ambaye kibarua chake kilionekana kuwa katika hatihati tangu walipofungwa 3-0 na Bournemouth.
Katika mchezo huo, Bruno alianzia benchi baada ya kuhoji hadharani mbinu zilizotumika katika kipigo kikali cha 4-1 dhidi ya Como, siku nne kabla.
Hata hivyo, kauli zake baada ya mchezo dhidi ya Roma zilikuwa za kujiamini zaidi kuliko za kulalamika au kulaumu.
“Hatuhitaji kuokoa kibarua cha mtu yeyote. Tumekuwa tukifanya kazi kwa bidii sana ili kujinasua kabisa kutoka katika hali hii.
“Imekuwa ngumu. Kumekuwa na uvumi mwingi kwenye vyombo vya habari, na uongo mwingi kuhusu mambo mengi yaliyotokea katika klabu hii. Kulikuwa na tetesi kwamba mimi na kocha tulihitaji kuweka mambo sawa; hakuna kitu kama hicho kilichotokea.”
“Kocha alichukua uamuzi wa kuniweka benchi kwa sababu sikuwa nikicheza katika kiwango kinachotakiwa. Watu wengi walihisi kuwa ilikuwa ni adhabu kutokana na maneno niliyoyasema. Ikiwa ilikuwa hivyo, basi ilikuwa sahihi pia,” alisema Bruno.
Carrick mwenyewe pia alipunguza uzito wa madai kwamba mabadiliko hayo ya matokeo yanaweza kuwa na manufaa kwake binafsi.
“Tumeonesha uthabiti mkubwa kama kikundi katika kukabiliana na changamoto zilizotukabili. Unapata fursa ya kufahamiana zaidi; wachezaji watagundua mambo kunihusu mimi, na mimi pia nimejifunza mengi kuwahusu wao, tabia zao, umuhimu wa jambo hili kwao, na kiwango cha kujitolea walicho tayari kukionesha,” alisema Carrick.




