Muziki

Boaz Danken kupamba The Night of Revelation 2026

DAR ES SALAAM:MWIMBAJI maarufu wa nyimbo za Injili nchini, Boaz Danken, anatarajiwa kuwa miongoni mwa waimbaji watakaopamba mkesha wa vijana wa kusifu na kuabudu unaojulikana kama ‘The Night of Revelation 2026’, utakaofanyika Januari 16, 2026 katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mabibo External.

Mkesha huo unakwenda sambamba na kaulimbiu isemayo “New Year, New Grace, New Hope”, ukiwa na lengo la kuwaandaa vijana kuukaribisha mwaka mpya kwa msingi wa kiroho, matumaini mapya na neema ya Mungu.

Akizungumza na Spoti Leo, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Usharika huo, Erick Kisaule, amesema mkesha huo ni ibada maalumu inayolenga kuwaunganisha vijana, kuwajenga kiroho na kuwaelekeza katika misingi sahihi ya kumcha Mungu.

“Mkesha huu una malengo makubwa ikiwemo kuwaunganisha vijana, kuwapa fursa ya kusifu na kuabudu pamoja, kujifunza neno la Mungu na kubadilishana mawazo ya kujenga kupitia mtumishi wa Mungu, Godluck Mushi, atakayehubiri neno,” amesema Kisaule.

Ameongeza kuwa mkesha huo pia unalenga kuwasaidia vijana kuukaribisha mwaka 2026 kwa mtazamo chanya, kutambua thamani yao katika jamii na kupanga pamoja kuyaombea malengo yao ya mwaka mpya, sambamba na kuliombea taifa liendelee kuwa na amani na mshikamano.

“Kupitia mkesha huu tunalenga pia kuwaepusha vijana na vishawishi visivyofaa vya mitaani kama matumizi ya dawa za kulevya, wizi na vitendo vingine vinavyohatarisha maisha yao ya sasa na baadaye,” amesisitiza.

Kisaule amesema kuwa hakutakuwa na kiingilio, na ibada hiyo iko wazi kwa watu wote. Mkesha utajumuisha kuimba, kusifu na kuabudu, kusikiliza neno la Mungu pamoja na maombi kwa watu wenye mahitaji na changamoto mbalimbali.

“Hii ni siku ya kipekee isiyopaswa kukoswa,” ameongeza.

Mbali na Boaz Danken, mkesha huo pia utawashirikisha waimbaji wengine wa nyimbo za Injili wakiwemo Essence of Worship na Elia Mtishibi, huku Mwl. Eng. Goodluck Mushi akiwa ndiye mtoa neno.

Kwa upande wake, Boaz Danken amewahimiza vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki ibada hiyo, akisema:
“Tuwe tayari kwa ibada ya kipekee ya kumsifu na kumtukuza Bwana. Mungu ana jambo kubwa kwa kizazi hiki.”

Mkesha wa The Night of Revelation 2026 utafanyika Januari 16, 2026 kuanzia saa 1:00 jioni katika KKKT Usharika wa Mabibo External.
Karibu wote kushiriki ibada hii ya kipekee ya usiku wa vijana.

 

Related Articles

Back to top button