Mwanamke anayetuhumiwa kumpiga Rihanna risasi hakuwa kichaa

LOS ANGELES:MWANAMKE anayetuhumiwa kufyatua risasi katika makazi ya mwimbaji Rihanna na mwenza wake, rapa A$AP Rocky, amepatikana kuwa na uwezo wa kiakili wa kusimama katika kesi na sasa mchakato wa jinai dhidi yake umeanza tena.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Los Angeles, Maria Cavalluzzi, alitoa uamuzi huo jana, Septemba 29, 2026, baada ya kesi hiyo kusimamishwa kwa muda wakati Ortiz akifanyiwa tathmini za kiakili.
Jaji pia aliamuru afikishwe tena mahakamani Jumatano leo kwa hatua inayofuata ya kesi inayomkabili.
Ortiz anakabiliwa na shtaka la kujaribu kumuua Rihanna pamoja na mashtaka 10 ya kushambulia kwa kutumia silaha ya moto aina ya semiautomatic.
Pia anakabiliwa na mashtaka matatu yanayohusiana na kufyatua risasi katika eneo lililokuwa na watu.
Licha ya yote hayo Ortiz amekana mashtaka hayo.
Kwa mujibu wa waendesha mashtaka, tukio hilo lilitokea Machi 8, 2026, katika eneo la Beverly Crest, Los Angeles ambapo Rihanna na A$AP Rocky walikuwa ndani ya trela aina ya Airstream wakati risasi zilipofyatuliwa kuelekea kwenye eneo lao la makazi.
Mamlaka zilisema angalau risasi 20 zilifyatuliwa kutoka kwenye bunduki aina ya AR-15, huku baadhi zikigonga trela ambayo Rihanna na A$AP Rocky walikuwemo. Risasi nyingine ziligonga ukuta wa eneo la chumba cha watoto wao. Hakuna mtu aliyejeruhiwa katika tukio hilo.
Ortiz, mwenye umri wa miaka 36 anatokea Orlando, Florida, alikamatwa siku hiyo hiyo baada ya polisi kumfuatilia.
Kwa mujibu wa taarifa za awali za mamlaka, alikuwa akikabiliwa na dhamana ya dola milioni 1.875. Ikiwa atapatikana na hatia, anaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.
Kwa sasa, sababu iliyomsukuma Ortiz kufanya tukio hilo bado haijawekwa wazi na mamlaka. Kesi hiyo itaendelea katika Mahakama Kuu ya Los Angeles baada ya jaji kurejesha rasmi mchakato wa jinai dhidi yake.




