Barcelona kuumana na Newcastle raundi ya 16

NYON:KLABU ya BARCELONA watakutana na Newcastle United katika hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya droo kufanyika leo kwenye makao makuu ya UEFA mjini Nyon, Uswisi.
Barça walikuwa na uwezekano wa kukutana na timu mbili ambazo ni Newcastle au PSG, na hatimaye wakapangwa dhidi ya klabu hiyo ya Ligi Kuu England. Newcastle wameingia hatua hii wakiwa na morali kubwa baada ya kuiondoa Qarabag kwenye Playoffs kwa ushindi mzito wa jumla ya mabao 9-3.
Timu hizi tayari zilishakutana mapema msimu huu kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya ligi uliopigwa St. James’ Park. Barcelona waliibuka na ushindi wa 2-1, huku Marcus Rashford akifunga mabao hayo.
Kwa kuwa Barcelona walimaliza kwenye nane bora, wamepata faida ya kupiga mechi ya pili nyumbani Camp Nou. Hata hivyo, mtihani mkubwa utakuwa kwenye mchezo wa kwanza England, hasa kwa presha na mazingira ya St. James’ Park.
Changamoto nyingine kwa kocha ni kukosekana kwa Frenkie de Jong, ambaye alikuwa mmoja wa wachezaji bora kwenye mchezo wa kwanza lakini safari hii hatakuwepo kutokana na majeraha.




