Aziz Ki aipasua kichwa Yanga

DAR ES SALAAM: SAKATA la Kiungo mshambuliaji wa timu ya taifa ya Burkina Faso, Stephane Aziz Ki limeibuka upya baada kudaiwa kuwa uongozi wa timu hiyo bado hawajafikia muafaka na nyota huyo kuongeza mkataba mpya klabuni hapo.
Rais wa Yanga, Eng. Hersi Said amethibitisha kuwa kiungo huyo bado hajasaini mkataba mpya na kubainisha kuwa mazungumzo yanaendelea hakuna kilichokamilika baina ya pande hizo mbili.
Aziz Ki alijiunga na Yanga, Julai 2022, mkataba wa miaka miwili, akitokea Asec Mimosas, akichukuwa nafasi ya mshambuliaji, Yacouba Sogne alipendekeza kusajiliwa kiungo huyo ambaye mkataba wake umefikia tamati msimu ulipita.
“Unajua tulimsajili kwa mkataba wa miaka miwili na huo mkataba umeisha, inamaana wanaomtaka wanazungumza naye moja kwa moja, upande wetu bado tunazungumza naye na hakuna kilichokamilika,” amesema Rais wa Yanga.
Hersi amekiri kuwa kiungo huyo ana ofa nyingi kutoka klabu mbalimbali zikijumuisha baadhi ya klabu kutoka Afrika Kusini, lakini mchezaji amewapa kipaumbele Yanga na kuendelea na mzungumzo na kupambana wanafanikiwa kumuongeza mkataba mpya.
“Yanga ipo kwenye wakati mgumu kumpoteza mchezaji kama huyo, bado hatujakata tamaa kwa sababu kuna asilimia kubwa ipo upande wetu kuweza kubaki na mchezaji huyo kikosini,” amesema Hesri.
Rais huyo amewatoa hofu mashabiki wa Yanga na kusema kuwa klabu hiyo ina uhusiano imara sana na Aziz na wamelifanyia kazi jambo hilo kama viongozi kuhakikisha anabaki ndani ya kikosi na kufikia malengo kwa msimu ujao.
Hivi karibuni kiungo huyo, aliwahi kusema kuwa anawapa kipaombele Yanga na anatarajia kubaki ndani ya klabu hiyo kwa vile ana jambo anatakiwa kulikamilisha akiwa na timu hiyo.