Kwingineko

Al-Hilal yalitetea bara Asia CWC

WASHINGTON: Klabu ya Al-Hilal ya Saudi Arabia imekuwa timu pekee ya bara Asia kutinga hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia la Klabu baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Pachuca alfajiri ya leo na kumaliza kampeni yao ya Kundi H bila kupoteza mchezo wowote huku wakijiandaa kukiruka kiunzi kingine kikubwa cha moto unaowaka wa Manchester City.

Tayari Al-Hilal walishaonesha kuwa wanaweza kushindana na timu bora zaidi duniani walipotoshana nguvu na timu kama Real Madrid na RB Salzburg kwenye sare ya 1-1 na 0-0 katika michezo yao miwili ya kwanza chini ya kocha mpya Simone Inzaghi.

Al-Hilal waliomaliza nafasi ya pili kwenye ligi kuu ya Saudi Arabia msimu uliomalizika Wameruhusu bao moja pekee katika mechi zao tatu za michuano hiyo inayoendelea nchini Marekani wakishea rekodi hiyo bora ya ulinzi ya hatua ya makundi sambamba na vigogo kama Paris St Germain na Monterrey.

Kocha wa kikosi hicho Simone Inzaghi amesema lilikuwa lengo lake kuifikisha klabu hiyo kwenye kundi la klabu 16 bora zaidi Duniani akisema kazi hiyo haikuwa rahisi lakini umoja ulio katika kikosi chake umewezesha hilo kutokea

“Lengo letu lilikuwa kuwa ndani ya kundi la timu bora zaidi ulimwenguni. Haikuwa kazi rahisi, lakini timu ilikuwa na umoja na muunganiko mzuri. Timu ilipigana wakati wote wa michezo yetu mitatu tukiwa na lengo kubwa, hatukuja hapa kujifurahisha tu, tumekuja hapa kucheza Kombe la Dunia na tulitaka kufikia hatua hii”.

“Sasa itabidi tucheze dhidi ya Manchester City, ni moja ya timu kubwa duniani. Aina hii ya michezo ni michezo ambayo unahitaji kujiimarisha na lazima ukomae kama timu, kwa hivyo ninajivunia.” – amesema Inzaghi

Al Hilal watakuwa na mtihani wenye maswali magumu mbele ya Manchester City saa 10 alfajiri ya Jumanne ya Julai 1 katika dimba la Camping World Stadium jijini Orlando, Florida. Man City ambayo haijapoteza mchezo wowote katika hatua ya makundi ya michuano hiyo ikishinda kwa 100% mech izote za makundi.

Related Articles

Back to top button