AFCON 2025: Ni Senegal na Morocco fainali Jumapili

RABAT: TIMU ya taifa ya Senegal itakutana na wenyeji Morocco katika fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 baada ya michezo miwili ya nusu fainali iliyojaa presha, ushindani mkali na matokeo yaliyopatikana kwa njia tofauti.
Morocco walijihakikishia nafasi ya kucheza fainali itakayofanyika Jumapili jijini Rabat baada ya kuibuka na ushindi wa penalti 4–2 dhidi ya Nigeria, kufuatia sare tasa ya dakika 120 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Prince Moulay Abdellah.
Awali jijini Tangier, mabingwa wa zamani Senegal walirejea fainali ya AFCON baada ya kuifunga Misri bao 1–0, ushindi uliokatisha ndoto za Mafarao hao kutwaa taji lao la nane barani Afrika.
Kwa upande wa Morocco walionesha nidhamu ya hali ya juu ya ulinzi dhidi ya Nigeria, huku mchezo ukikosa ubunifu wa kushambulia lakini ukijaa tahadhari na umakini kwa pande zote mbili.
Licha ya Nigeria kujaribu kushambulia kwa nyakati tofauti, safu ya ulinzi ya Atlas Lions ilisimama imara kwa dakika zote 120, kabla ya mchezo kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti.
Morocco walitumia vyema mikwaju yao, wakifunga penalti nne kati ya tano, huku Nigeria wakifunga penalti mbili pekee, ushindi uliowapeleka Morocco fainali yao ya kwanza ya AFCON tangu walipotwaa ubingwa mwaka 1976 wakiwa wenyeji.
Kwa upande wao Senegal walipata ushindi mwembamba lakini muhimu wa bao 1–0 dhidi ya Misri katika mchezo uliochezwa kwa ushindani mkubwa.
Bao la mshambuliaji nyota Sadio Mane liliipa Senegal ushindi huo, wakionesha uzoefu, subira na ubora wao dhidi ya Misri yenye historia kubwa kwenye michuano hiyo.
Fainali ya AFCON 2025 itachezwa Jumapili, Januari 18, katika Uwanja wa Prince Moulay Abdellah, Rabat, ambapo Morocco watajaribu kuandika historia nyumbani dhidi ya Senegal wanaotaka kurejesha taji walilotwaa mwaka 2021.
Mechi ya mshindi wa tatu itawakutanisha Nigeria na Misri Jumamosi, Januari 17, katika Uwanja wa Mohammed V, Casablanca.




