Simba amepita mule mule!

MOROGORO: KLABU ya Simba imeendelea na utaratibu wao wa kila msimu kutambulisha jezi zao kwa kutumia hifadhi za utalii, safari hii wamezindulia katika hifadhi ya Mikumi.
Msimu uliopita, jezi za Simba zilizinduliwa kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro, mlima mrefu zaidi Afrika! Nilipata fursa ya kusindikiza kibegi kuelekea Uhuru Peak.
Jezi za msimu wa 2024/25 zimezinduliwa nyumbani kwa Mnyama, kwenye Mbuga ya Wanyama ya Mikumi iliyopo Mkoa wa Morogoro, muendelezo wa kuiunga mkono serikali katika kutangaza utalii kupitia michezo.
Msafara wa Simba ulifika katika Hifadhi za Mbuga ya Wanyama Mikumi saa 8:30 kabla ya kuingia katika uwanja wa mpira ambapo kulikuwa na mchezo wa wafanyakazi wa hifadhi hiyo dhidi ya viongozi wa Simba.
Walioongoza kikosi cha viongozi wa Simba ni Mtendaji Mkuu, Imani Kajula, Mwasibu wa Simba, Suleiman Kahumbu na Mzabuni ambaye anatengeneza jezi za Simba kwa msimu wa pili mfululizo, Omary Sunderland.
Saa 9:05 alasiri uongozi huo ulizindua jezi za Simba zitatumika kwa msimu mpya wa mashindano ndani ya hifadhi ya Mikumi ambazo ni rangi nyekundu (nyumbani), jezi ya rangi nyeupe (ugenini) na jezi ya tatu ambayo ni rangi ya bluu.