
DAR ES SALAAM: WAKATI Simba ikiwa katika hatua za mwisho kumuongezea mkataba kipa wao, Ayoub Lakred makipa wengine watatu wa timu hiyo wako katika sintofahamu ya kupunguzwa kikosini.
Makipa hao Ally Salum, Hussein Abel na Aishi Manula kati ya hao mmoja wapo atakutana na panga la kuondolewa kwenye kikosi cha timu hiyo kwa msimu ujao.
Imeelezwa kuwa viongozi wa Simba wapo kwenye mazungumzo ya kumbakiza kikosini Ayoub huku wakiwa na mchakato wa kupunguza idadi ya makipa hao na huenda mmoja wa makipa watatu atakutana na ‘Thank You’.
Kigogo ndani ya Simba, amesema wanahitaji kuwa na idadi ya makipa wachache huku wakikaribia kumalizana na Ayoub kwa mkataba wa mwaka mmoja.
“Kuna mambo mawili yanafanyika ikiwemo mchakato wa kumuongezea mkataba kipa wetu Ayoub lakini kupunguza idadi ya makipa tuliokuwa nao, msimu ujao tunahitaji kubaki na watatu,” amesema mtoa habari huyo kutoka ndani ya klabu hiyo.
Alipotafutwa Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amewataka mashabiki kupunguza presha na kuwa watulivu kwa sababu kuna maboresho makubwa yanafanyika kila idara ikiwemo safu ya ulinzi, viungo na washambuliaji.
“Kuhusu Ayoub viongozi wanaendelea na mazungumzo ya kuhakikisha wanamuongezea mkataba nyota huyo na tupo kwenye hatua nzuri, matarajio yetu msimu ujao kuwepo kwenye kikosi cha Simba,” amesema Ahmed.