Habari Mpya

Corazone Aquino ataka kuipa Simba Queens taji la Afrika

“TAJI la Cecafa, tuzo ya mchezaji bora na kufuzu kucheza michuano ya Kombe la Ligi ya Mabingwa wa Afrika ni majaliwa ya Mungu.”

Hayo ni maelezo ya kiungo wa timu ya taifa ya wanawake ya Kenya, Harambee Starlets, Corazone Aquino mara baada ya kutwaa taji la Cecafa na kuisaidia Simba Queens kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa wa Afrika kwa upande wa akina mama.

Aquino aliyekuwa na furaha isiyo na kifani alitwaa taji hilo la Cecafa baada ya kuisaidia Simba Queens baada ya kufunga kwa penalti bao pekee katika mchezo dhidi ya She Corporate ya Uganda katika fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Kiungo huyo mwenye uzoefu mkubwa alifunga bao hilo pekee katika dakika ya 47 na kumuwezesha kocha Sebastian Nkoma kufanikiwa kutwaa taji hilo katika ardhi ya nyumbani.

Aquino pia aliiwezesha Simba Queens kutoa mfungaji bora baada ya kufunga mabao matano, huku kiatu cha dhahabu kikienda kwa Loza Abera wa Benki Kuu ya Ethiopia (CBE) iliyomaliza ya tatu katika mashindano hayo.

“Haya ni mafanikio makubwa sana kwangu, timu yangu na hata kwa nchi yangu Kenya. Kocha Nkoma alinisaidia kuzoea haraka katika timu hii na kunifanya kuonesha kipaji changu vizuri,” anasema katika mahojiano na Nation Sport hivi karibuni.

Kiungo huyo wa Harambee Starlets alijiunga na Simba Queens au Wekundu wa Msimbazi Juni 22 kutoka timu ya Gaspo inayoshiriki Ligi Kuu ya wanawake ya Kenya.

Msimu uliopita kiatu cha dhahabu kilikwenda kwa mchezaji wa Ligi Kuu, Topister Situma aliyejiunga na Simba Queens Julai 6, ambaye ali- ingia uwanjani dakika 10 za mwisho.

Aquino mwenye umri wa miaka 23 kwa sasa anaangalia kushinda taji la wanawake la Ligi ya Mabingwa wa Afrika. Mashindano hayo ni ya pili mwaka huu na itafanyika nchini Morocco kati ya Oktoba na Novemba.

“Ninajiamini sana, tunaweza kufanya vizuri na kushinda taji la Ligi ya Mabingwa wa Afrika. Hata hivyo, hii inahitaji juhudi zaidi kutoka kwa wachezaji wenzangu na benchi la ufundi. Tutapambana kushindana kwa sababu inawezekana na kikosi chetu pia ni kizuri,” aliongeza Aquino.

BARBARA ANENA

Ofiza Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia walifurahishwa na matokeo hayo ya Simba Queen na kuahidi kuisaidia timu hiyo kwa ajili ya maandalizi ya mashindano hayo.

“Ninajivunia wasichana wetu kwa sababu wameipeperusha vizuri bendera yetu. Hii inadhihirisha kuwa Tanzania inazidi kuimarika na kama klabu tunatakiwa kuwasapoti wakati wakianza maandalizi kwa ajili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa,” alisema Gonzalez.

Vihiga Queens ilishinda taji la Cecafa mwaka 2021, lakini haikushiriki katika mashindano hayo ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika baada ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) kuifungia Kenya baada ya serikali kuingilia masuala ya soka.

KOCHA NKOMA

Kocha wa Simba Queens, Sebastian Nkoma alielezea furaha yake na kuahidi kuiandaa timu vizuri kwa ajili ya mashindano hayo ya wanawake ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.

“Tulifanya vizuri katika mashindano haya na nimefurahishwa sana na ushindi. Sasa kazi kubwa iliyopo mbele yetu ni kuiandaa timu vizuri kwa ajili ya kushindana na timu bora Afrika. Ndoto yetu ni kuleta nyumbani taji la Ligi ya Mabingwa wa Afrika,” alisema Nkoma.

Naye kocha wa She Corporate, Charles Ayieko alikipongeza kikosi chake kwa kupambana hadi kufuzu kwa fainali na aliipongeza Simba Queens kwa kutwaa taji hilo katika ardhi ya nyumbani.

“Simba ilistahili ubingwa kwani walikuwa na timu nzuri na kocha mzuri. Tulifanya kosa moja na waliweza kutumia nafasi vizuri na kutuadhibu. Nawapongeza wasichana wangu, huu ni mchezo mzuri mbele ya mashabiki waliofurika uwanjani,” anasema kocha huyo wa Uganda.

Mshambuliaji wa Ethiopia, Loza Abera amekuwa mfungaji bora baada yakutingisha nyavu mara 11.

Hilo lilikuwa bao la tano kwa Aquino katika mashindano hayo. Mbali na kutwaa taji hilo, Simba Queens pia walipewa zawadi ya Dola za Marekani 30,000 wakati Waganda, She Corporate walizawadiwa Dola 20,000.

Katika mchezo wa kusaka mshindi watatu, timu ya Ethiopia ambao ni washindi wa pili mwaka jana, Benki Kuu ya Ethiopia (CBE) waliifunga AS Kigali ya Rwanda kwa mabao 3-1 na kutwaa Dola za Marekani 5,000.

MABAO YA AQUINO

Aquino pia alifunga mabao mawili wakati Simba Queens ikishinda 5-1 dhidi ya AS Kigali katika nusu fainali. Pia alipata bao katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya She Corporate katika mchezo wa Kundi B na Yei Joint Stars ya Sudan Kusini.

HISTORIA YAKE

Aquino awali aliwahi kuzichezea timu ya Ligi Kuu ya Ureno ya Atletico Ouriense kati ya mwaka 2020 na 21 kabla hajatua katika timu ya Ligi Kuu ya Kenya ya Gaspo msimu wa mwaka 2021/22.

Jina lake hilo ni lile la rais wa zamani wa Ufilipino, Corazon Aquino na awali alivuma tangu akiwa katika Makongeni High School na Olympic High School ambako alishinda taji la taifa mwaka 2013.

Alikuwa nahodha wa timu ya taifa ya wachezaji wenye umri chini ya miaka 17 mwaka 2014 na tangu wakati huo aliopandishwa hadi katika timu ya taifa ya wanawake ya wakubwa, Harambee Starlets, ambako alijiunga mwaka 2016.

Related Articles

Back to top button