Moro Youth yatamba ukuzaji vipaji nchini

TAASISI ya Kukuza na Kulea Vipaji vya Soka kwa Vijana Morogoro (Moro Youth) imefanikiwa kuibua na kukuza vipaji wa soka kwa mamia ya vijana ambao miongoni mwao wamefanikiwa kucheza timu ya Taifa ya wakubwa na wengine timu ya Taifa ya vijana.
Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Profesa Madundo Mtambo alisema hayo ,wakati wa bonaza la mchezo wa soka kati ya timu ya Moro All Stars dhidi ya Moro Kids kwa ajili ya kuadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Taasisi hiyo mkoani Morogoro.
Profesa Madundo ambaye aliwahi kuchezea timu za soka ya Reli Kiboko cha Vigogo nyakati hiyo pamoja na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) , kwa sasa ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utafiti na Uendelezaji Viwanda Tanzania (TIRDO).
Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, alisema kuwa hadi sasa Taasisi hiyo ina vijana zaidi ya 200 katika kituo hicho.
“ Miaka 25 ya Kituo hiki vijana wengi wamnepita kwetu walikuwa na miaka 10 kwa sasa wamefikisha zaidi ya miaka 25 na wanaumri mkubwa “ alisema Profesa Madundo
Profesa Madundo alisema Kituo hicho kimepata mafanikio makubwa ikiwa na kutoa zaidi ya vijana 17 waliopitia ambao walikuwa kwenye timu ya Taifa ya wakubwa na vijana 19 kwenye timu ya Taifa ya Vijana .
“ Bado tunavijana wengi ambao wapo kwenye timu za ligi kuu , ligi daraja la kwanza na ligi zingine za ngazi mbalimbali “ alisema Profesa Madundo
Profesa Madundo aliwashukuru wadau mbalimbali wa mpira wa miguu wa mkoa wa Morogoro , serikali ya mkoa huo na Meya wa Manispaa ya Morogoro kwa kuwa karibu na Kituo hicho kwa kuwaunga mkono.
Pia aliwashukuru baadhi ya wachezaji waliopitia kwenye Kituo kwa kutenga muda wao kwa kufika kuungana katika bonaza la maadhimisho ya miaka 25 ya kituo hicho.
Naye mchezaji anayetokana na zao la Kituo hicho , Shomari Kapombe ambaye kwa sasa ni mchezaji nguli wa timu ya Simba alisema, ni jambo la furaha kujumuisha na wachezaji waliotokana na kituo hicho na kucheza kwenye uwanja wa SabaSaba ambao uliwakuza chini ya walimu mbalimbali wa soka wa kituo hicho.
“ Ni jambo la furaha kukutana na wenzagu tunaotokana na kituo hiki na kumecheza mpira tena kwenye uwanja huu ambao ndiyo chimbuko letu sote , tumeonesha kipaji chetu cha soka nikiwemo mimi mwenyewe na pia kukutana na viongozi wetu “ alisema Kapombe
Alisema wachezaji wengi anaotamba katika timu mbalimbali nchini ni zao la kituo hicho , hivyo aliamua kuja kuwatia moyo waliopo kwa sasa kuwa wasikate tamaa ila waongeze bidiii.
“ Ninawambia vijana kuwa neno mafanikio ni neno dogo lakini linauzito mkubwa , na mafanikio kuyapata inaabidi kupambana , upambanie hilo neno mafanikio kwa kuweka malengo yanayofikiwa bila kusahu nidhamu ndani ya mchezo nan je ya mchezo” alisema Kapombe
Taasisi hiyo imezalisha wachezaji wengi wanawika katika medani ya soka nchini wakiwemo Shomari Kapombe, Kibwana Shomari, Mzamiru Yassin , Shizya Kichuya , Dickson Job , Zawadi Mauya , Kassian Ponera, Jaffary Kibaya na Edward Christopher ambao wengi walishiriki katika bonaza hilo ambalo liliambatana na utoaji wa tuzo kwao.