Mastaa

Zuchu amvaa Nandy, adai kumvumilia kwa muda mrefu

DAR ES SALAAM: MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Zuhura Othuman ‘Zuchu’, ameibua mjadala mkubwa mitandaoni baada ya kumshambulia kwa maneno msanii mwenzake, Faustina Charles ‘Nandy’, akidai kuwa amekuwa akivumilia vitendo mbalimbali anavyodai kufanyiwa kwa muda mrefu.

Zuchu ametoa tuhuma hizo kupitia ukurasa wake wa Instagram, ambako ameandika ujumbe mrefu akieleza mambo mbalimbali ambayo anadai yamekuwa yakitokea baina yao, ikiwamo suala la Nandy kumtoa msanii Yammi kama mpinzani wake wa kimuziki.

Katika ujumbe huo, Zuchu amedai kuwa hatua ya Nandy kumtangaza Yammi kama msanii wa kumzidi kimuziki ilimfanya kuwa kitovu cha ushindani wao, huku akieleza kuwa sasa hali imebadilika na kile alichodai kilikuwa sehemu ya ushindani huo kinaonekana kumrudia mwenyewe.

“Alimtoa Yammi akijinadi kabisa kuwa huyu ndiye kiboko yake Zuchu, mkachukua mastaa wa mitindo mpaka kumpeleka saluni ninazosuka mimi, lakini sasa kinyago chake mwenyewe kinamtisha,” aliandika Zuchu.

Aidha, Zuchu amedai kuwa kumekuwa na matukio mengine yaliyohusisha watu wanaofanya kazi naye, akiwamo aliyekuwa meneja wake Doris, pamoja na masuala ya biashara na huduma za urembo, ambayo anasema yalichangia uamuzi wake wa kujitenga ili kuepusha migogoro.

Ameeleza pia kuwa amekuwa akichagua kukaa kimya licha ya kile anachodai kuwa ni vitendo vya kumchokoza na kuibua ushindani usio wa lazima.

Katika sehemu nyingine ya ujumbe wake, Zuchu amezungumzia suala la kujitangaza kwa shughuli zake, akidai kuwa baadhi ya hatua zake zimekuwa zikifuatwa na Nandy kwa namna ambayo anaiona kama ushindani wa moja kwa moja.

Akitolea mfano, ametaja kutangaza kwa shughuli zake za kimuziki na madai ya Nandy kutangaza tamasha lake bila kuweka bayana tarehe wala wasanii watakaoshiriki.

Zuchu ameendelea kueleza kuwa pamoja na kuwa na sababu nyingi za kuzungumza, amekuwa akijizuia kwa kuwa haoni faida ya kuanzisha mijadala inayoweza kuathiri shughuli zake.

Hata hivyo, amedai kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakimtetea Nandy bila kufahamu mambo anayodai kuyapitia, huku akilalamikia kile anachokiona kuwa ni kutokuwepo kwa usawa katika namna wasanii hao wanavyotazamwa wanapofanya mambo yanayofanana.

Ameongeza kuwa mafanikio ya mtu mwingine hayapaswi kuwa sababu ya kumfanya mtu ajihusishe na ushindani usioisha, akigusia pia suala la ununuzi wa gari lake na madai kwamba Nandy alichukua hatua ya kutafuta nyumba katika mazingira aliyoyaona kama mashindano.

Katika hitimisho la ujumbe wake, Zuchu amemshutumu Nandy kwa kile alichokiita unafiki na kudai kuwa amekuwa akijikita zaidi kufuatilia hatua zake kuliko kuendeleza shughuli zake.

Kauli hizo zimeibua mjadala miongoni mwa mashabiki wa muziki wa Bongo Fleva, huku wengi wakisubiri kuona kama Nandy atatoa ufafanuzi kuhusu tuhuma hizo.

Related Articles

Back to top button