Ligi Kuu

Fadlu: MC Alger lazima ajilinde dakika 90

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Yanga, Fadlu Davids, amesema anataka kuibana MC Alger katika eneo lake kwa muda wote wa mchezo ili kuipa timu hiyo nafasi ya kutengeneza mashambulizi na kupata pointi tatu muhimu katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Fadlu amesema tayari benchi lake la ufundi limeichambua MC Alger na kutazama baadhi ya michezo yake, akibainisha kuwa timu za Afrika Kaskazini zinapocheza ugenini huwa na tabia ya kujilinda zaidi, kujipanga vizuri na kutumia mashambulizi ya kushtukiza.

Amesema kutokana na uchambuzi huo, Yanga inajiandaa kutumia mfumo wa kushambulia utakaomlazimisha mpinzani kubaki katika eneo lake la ulinzi kwa dakika zote 90 ili kuongeza nafasi za kufunga mabao.

“Tunapokuwa na taarifa kuhusu mpinzani, tunapaswa kutekeleza mfumo wa kushambulia utakaomfanya aendelee kujilinda kwa dakika 90. Akija kujilinda, tutamlazimisha ajilinde. Jukumu letu ni kushambulia, kufunga na kuhakikisha tunapata pointi tatu,” amesema Fadlu wakati akizungumza na waandishi wa Habari leo.

Amesisitiza kuwa kwa sasa mawazo yake yote yapo katika mchezo wa nyumbani dhidi ya MC Alger na si wapinzani wengine wa kundi hilo, akiwemo mabingwa wa Tunisia na Misri, ambao watakutana nao baadaye.

Fadlu amesema anafahamu MC Alger kutokana na kukutana nayo msimu uliopita, wakati Yanga ilipofanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali, hivyo uzoefu huo utasaidia katika maandalizi ya mchezo huo.

Amesema pia anaamini uwepo wa mashabiki wa Yanga uwanjani utawapa nguvu wachezaji wake na kuufanya mchezo kuwa mgumu kwa wapinzani, akitarajia mashabiki kujitokeza kwa wingi na kutengeneza mazingira magumu kwa MC Alger.

Mwisho

Related Articles

Back to top button