Michezo Mingine

Ferrari yawaka moto baada ya Hamilton na Leclerc kugongana

LAS VEGAS: TIMU ya Ferrari imeelezea kutoridhishwa kwake na kitendo cha madereva wake Lewis Hamilton na Charles Leclerc kugongana katika mashindano ya Formula One (F1) Grand Prix ya Las Vegas, ikikitaja kuwa hakikubaliki kabisa.

Tukio hilo lilitokea zikiwa zimesalia mizunguko 22 kabla ya kumalizika kwa mbio hizo, baada ya Leclerc kumgonga Hamilton na kumsababisha kuzunguka akiwa kwenye njia ya mashindano, jambo lililoathiri matokeo ya madereva wote wawili.

Leclerc alipewa adhabu ya kuongeza sekunde 10, hali iliyomfanya amalize katika nafasi ya 10, huku Hamilton akimaliza nafasi tatu mbele yake.

Mbio hizo zilishuhudiwa zikishindwa na Max Verstappen wa Red Bull, huku madereva wa McLaren wakifanikiwa kushika nafasi za jukwaani.

Akizungumzia tukio hilo, mkuu wa timu ya Ferrari, Frederic Vasseur, alisema kitendo hicho hakikubaliki na kinaonyesha kutoheshimu timu pamoja na wadhamini wake.

Vasseur alifichua kuwa madereva hao walikuwa tayari wameonywa baada ya tukio jingine lililotokea katika mashindano ya Mexico, ambapo kutokuelewana kwao kulichangia kupoteza nafasi nzuri ya ushindi.

Alisema Ferrari ilikuwa imewapa maelekezo ya kuzingatia maslahi ya timu wanapokuwa wakishindana wao kwa wao, lakini tukio la Las Vegas limeonyesha kuwa tatizo hilo bado halijatatuliwa.

Kwa upande wake, Hamilton alisema tukio la aina hiyo halipaswi kutokea kabisa, huku akisisitiza kuwa sasa ni jukumu la Ferrari kushughulikia suala hilo.
Bingwa huyo mara saba wa dunia pia alikanusha madai kwamba amekuwa akiomba kupewa hadhi ya dereva namba moja ndani ya timu hiyo.

Leclerc naye alikiri kuwa alifanya makosa na kusema adhabu aliyopewa inaonyesha kuwa waamuzi walimwona kuwa na hatia katika tukio hilo.

Aidha, Mfaransa Vasseur amesema atakutana na madereva hao ili kujadili kilichotokea baada ya hali ya hasira za mara baada ya mashindano kutulia.

Mvutano kati ya Hamilton na Leclerc umekuwa ukiongezeka katika kipindi cha pili cha msimu huu, huku kukiwa na tofauti za kimtazamo kuhusu mbinu za mbio, mikakati ya timu na namna wanavyopaswa kushindana wakiwa upande mmoja.

Sasa macho yanaelekezwa katika mazungumzo ya ndani ya Ferrari, huku timu hiyo ikihitaji kutatua tofauti hizo ili kuepusha migongano mingine inayoweza kuathiri matokeo yake katika mashindano yajayo.

Related Articles

Back to top button