Simba inapima uzito wa Gor Mahia

DAR ES SALAAM: SIMBA huenda ikacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya mabingwa wa soka nchini Kenya, Gor Mahia, jijini Nairobi wakati huu wa mapumziko ya kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), baada ya kupokea mwaliko kutoka kwa klabu hiyo.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema uongozi wa klabu hiyo bado unafanya tathmini ya mwaliko huo kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu ushiriki wa timu katika mchezo huo.
Amesema mara baada ya maamuzi kukamilika, klabu itawasiliana na Gor Mahia na kuwapa taarifa mashabiki wake kuhusu hatua iliyofikiwa.
“Bado maamuzi ya mwisho hayajafanyika. Tukishakuwa tayari tutawajulisha Gor Mahia, sambamba na kuwajulisha Wanasimba tumefikia wapi kuhusu mwaliko huo pamoja na mchezo,” amesema.
Ahmed amesema wachezaji wa Simba wamepewa mapumziko hadi Novemba 9, lakini maandalizi ya kuelekea hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na kuendelea kwa Ligi Kuu ya NBC tayari yameanza.
Katika maandalizi hayo, Simba pia inaendelea na mazungumzo na Serikali kuhusu marekebisho ya Uwanja wa Uhuru kufuatia mapendekezo yaliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ili uweze kutumika katika michezo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Amesema wamezungumza na wamiliki wa uwanja huo ambao ni Serikali, ili kuona uwezekano wa kufanyika kwa marekebisho hayo kwa wakati kabla ya mchezo wao wa kwanza dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Ameeleza kuwa endapo mapendekezo ya CAF yatatekelezwa kwa wakati, Simba itautumia Uwanja wa Uhuru kama uwanja wake wa nyumbani katika michuano hiyo.




