Mastaa

Alikiba azungumzia talaka ya Amina, “ndoa ni maisha binafsi” 

DAR ES SALAAM:MSANII nyota wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba maarufu kama Alikiba, amekwepa kuweka wazi iwapo tayari amempa talaka mke wake, Amina Khalef, raia wa Kenya, kufuatia taarifa za mwanamke huyo kuwasilisha ombi la kuvunjwa kwa ndoa yao.

Akizungumzia suala hilo, Alikiba amesema maisha yake ya ndoa ni jambo binafsi ambalo halipaswi kuwa mjadala wa kila mtu, akisisitiza kuwa si kila jambo linalohusu familia yake anapaswa kulijibu hadharani.

“Kiukweli mnaelewa hili swali siwezi kulijibu, lipo kibinafsi zaidi na maisha yangu ya ndoa hayamhusu kila mtu,” amesema Alikiba.

Hata hivyo, msanii huyo aliongeza kauli iliyozua mjadala alipogusia tofauti zinazoweza kujitokeza kati ya wanandoa, akihusisha hali hiyo na kipindi fulani cha kila mwezi.

“Na pia wanawake wanakuwa na siku tano za kugombana na wanaume zao kila mwezi, zikisha mnakuwa na amani, nadhani tumeelewana,” amesema.

Kauli hiyo imekuja wakati taarifa kuhusu uwezekano wa kuvunjika kwa ndoa yake na Amina zikiendelea kuibua maswali kwa mashabiki wa mwanamuziki huyo, ambao wamekuwa wakisubiri kufahamu hatma ya uhusiano wao.

Alikiba na Amina Khalef walifunga ndoa Aprili 2018 na wamejaliwa kupata watoto wawili.

Hadi sasa, Alikiba hajatoa ufafanuzi wa moja kwa moja kuhusu iwapo talaka imeshatolewa au hatua za kisheria za kuvunja ndoa zimekamilika, akibaki kusisitiza kuwa suala hilo ni sehemu ya maisha yake binafsi.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button