Ligi Daraja La Kwanza

Mtoto wa Ronaldo aitwa timu ya taifa Ureno

LISBON: MTOTO wa kwanza wa staa Cristiano Ronaldo, Cristiano Ronaldo Jr., kwa mara ya kwanza ameitwa katika timu ya taifa ya Ureno ya vijana wenye umri chini ya miaka 17.

Ronaldo Jr., 16, amejumuishwa katika kikosi cha wachezaji 23 kilichoitwa na Kocha Mkuu, Filipe Ramos kwa ajili ya mechi zijazo za kufuzu michuano ya Kombe la Ulaya (UEFA Euro U17).

Hatua hiyo, ni muendelezo mzuri kwake baada ya awali kung’ara vikosi vya U15 na U16 vya Ureno.

Katika makundi yote mawili ya umri, mshambuliaji huyo anayekipiga Al Nassr ya Saudia, amecheza mechi 13 na kufunga mabao matano.

Taarifa zinafafanua kuwa kinda huyo pia amefanya vizuri katika ngazi ya klabu, akifunga mabao matatu katika mechi saba alizoichezea timu ya vijana ya Al Nassr msimu huu.

Aidha, Ureno itaanza kampeni yake ya kufuzu UEFA Euro dhidi ya Andorra, Novemba 11, kabla ya kukabiliana na Bulgaria mnamo Novemba 14. Mechi ya mwisho itakuwa dhidi ya Serbia, Novemba 17, mwaka huu.

Mechi zote tatu zimepangwa kufanyika katika kituo cha mazoezi cha Shirikisho la Soka la Ureno, Oeiras.

Related Articles

Back to top button