Udinese yamfukuza kocha, Zanetti akabidhiwa mikoba

UDINE: KLABU ya Udinese imekuwa timu ya tano katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kubadilisha kocha msimu huu baada ya kumfuta kazi Kosta Runjaic kufuatia mwenendo mbaya wa matokeo ya timu hiyo.
Uamuzi huo ulitangazwa Jumatatu, Novemba 2, 2026, huku klabu hiyo ikimteua Paolo Zanetti kuwa kocha mpya hadi mwisho wa msimu.
Runjaic amepoteza nafasi yake baada ya Udinese kupata matokeo mabaya katika michezo ya hivi karibuni, ambapo timu hiyo imepoteza michezo saba kati ya nane iliyocheza katika ligi. Mfululizo huo wa matokeo umeifanya klabu hiyo kujikuta katika eneo la hatari ya kushuka daraja, tofauti na misimu miwili iliyopita ambayo ilimaliza katika nafasi za katikati ya msimamo wa ligi.
Kipigo cha mabao 5-2 dhidi ya Roma katika uwanja wa nyumbani mwishoni mwa wiki iliyopita kimeelezwa kuwa moja ya sababu zilizochochea uongozi wa Udinese kuchukua hatua ya kumtimua kocha huyo. Roma, ambayo imeanza msimu kwa ushindani mkubwa katika mbio za ubingwa, iliitandika Udinese na kuongeza presha kwa benchi la ufundi.
Katika taarifa yake rasmi, Udinese ilisema imefikia uamuzi wa kuachana na Runjaic baada ya kufanya kazi pamoja kwa zaidi ya miaka miwili, kipindi ambacho kilihusisha mafanikio ya baadhi ya malengo muhimu yaliyokuwa yamewekwa na klabu. Hata hivyo, matokeo ya hivi karibuni yamefanya uongozi kuona umuhimu wa kufanya mabadiliko ili kujaribu kurejesha ushindani wa timu.
Kocha mpya Paolo Zanetti anakabidhiwa jukumu la kuifufua Udinese ambayo imekusanya pointi tano pekee katika michezo 10 ya Serie A msimu huu. Zanetti ana uzoefu wa kuifundisha timu za Venezia, Empoli na Verona, hivyo anatarajiwa kutumia uzoefu huo kuisaidia klabu hiyo kujinasua katika nafasi za kushuka daraja.
Runjaic anaungana na makocha wengine waliopoteza ajira zao katika Serie A msimu huu, akiwemo Fabio Grosso wa Fiorentina, Domenico Tedesco wa Bologna, Carlos Cuesta wa Parma na Davide Nicola wa Venezia. Mabadiliko hayo yanaendelea kuonesha ushindani na presha kubwa inayowakabili makocha katika ligi hiyo, huku Udinese sasa ikitarajia kupata matokeo bora chini ya Zanetti katika kipindi kilichosalia cha msimu.




