Tennis

Zverev awa mchezaji namba moja duniani wa tenisi

UJERUMANI: MCHEZAJI wa tenisi kutoka Ujerumani, Alexander Zverev, ameingia katika historia baada ya kufanikiwa kuwa mchezaji namba moja duniani kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya mchezo huo, kufuatia ushindi wa seti mbili kwa bila dhidi ya Tallon Griekspoor wa Uholanzi katika mashindano ya Vienna Open.

Zverev, mwenye umri wa miaka 29, alishinda kwa seti 6-4, 7-5 katika mchezo wa hatua ya 16 bora siku ya Alhamisi, matokeo yaliyomuwezesha kutwaa nafasi ya kwanza katika orodha mpya ya viwango vya ATP inayotarajiwa kutangazwa Jumatatu ijayo.

Ingawa tayari alikuwa amehakikisha kumaliza msimu wa mwaka 2026 akiwa kileleni mwa viwango hivyo, kutokuwepo kwa Jannik Sinner wa Italia kutokana na jeraha la goti kulifungua njia kwa Mjerumani huyo kumpiku na kutwaa rasmi nafasi hiyo.

Mwaka huu umekuwa wa mafanikio makubwa kwa Zverev, ambaye alivunja rekodi yake ya kusubiri kwa muda mrefu mataji makubwa baada ya kutwaa ubingwa wa French Open na US Open.

Kwa mafanikio hayo, Zverev anakuwa mchezaji wa 30 katika historia ya tenisi ya wanaume kufikia nafasi ya kwanza duniani tangu mfumo wa viwango vya ATP ulipoanzishwa mwaka 1973.

Pia, atakuwa mchezaji wa pili mwenye umri mkubwa zaidi kufikia nafasi hiyo kwa mara ya kwanza, akiwa na miaka 29 na siku 196, nyuma ya Muaustralia John Newcombe.

Safari yake ya kutwaa nafasi hiyo haikuwa rahisi, kwani katika mchezo wake wa kwanza dhidi ya Mhispania Martin Landaluce alilazimika kuokoa nafasi nne za ushindi kabla ya kuibuka mshindi.

Hata hivyo, ushindi dhidi ya Griekspoor ulimhakikishia kuandika historia mpya kabla ya mashindano ya mwisho wa msimu ya ATP Finals yatakayofanyika mwezi ujao.

Related Articles

Back to top button