JAY-Z kutumbuiza Super Bowl LXI

LOS ANGELES: MSANII wa muziki wa hip-hop na mfanyabiashara kutoka Marekani, Shawn Corey Carter maarufu Jay-Z, anatarajiwa kutumbuiza katika kipindi cha mapumziko cha fainali ya Super Bowl LXI itakayofanyika Februari 14, 2027, jijini Los Angeles, Marekani.
Taarifa ya Shirikisho la Soka la Marekani (NFL) iliyotolewa Jumatatu, Oktoba 26, 2026, imethibitisha ushiriki wa msanii huyo katika hafla hiyo inayotazamwa na mamilioni ya mashabiki wa michezo na burudani duniani.
Jay-Z, amekuwa na mchango mkubwa katika kuandaa burudani za Super Bowl kupitia kampuni yake ya Roc Nation, iliyokuwa ikisimamia utayarishaji wa maonesho hayo tangu mwaka 2020.
Kamishna wa NFL, Roger Goodell, alisema alipofikia makubaliano na Roc Nation kuhusu utayarishaji wa maonesho hayo, alikuwa na ombi moja kwamba siku moja Jay-Z mwenyewe apande jukwaani, pale atakapoona muda muafaka umefika.
Goodell alieleza kufurahishwa na uamuzi huo, akisema mashabiki duniani watapata fursa ya kufurahia ubunifu, sanaa na mchango wa Jay-Z katika utamaduni wa muziki kupitia jukwaa hilo kubwa.
Hata hivyo, taarifa ya NFL haikubainisha iwapo Jay-Z atakuwa msanii pekee wa kutumbuiza katika kipindi hicho. Tangazo hilo limekuja baada ya msanii huyo kufanya maonesho mawili jijini Los Angeles wiki iliyopita, ikiwa ni sehemu ya ziara ya kuadhimisha miaka 30 tangu kutolewa kwa albamu yake ya kwanza, ‘Reasonable Doubt.’
Akizungumzia nafasi hiyo, Jay-Z alisema safari yake kutoka kutengeneza albamu yake ya kwanza hadi kufikia jukwaa la Super Bowl ni ndoto inayotimia. Katika maonesho yake ya hivi karibuni Los Angeles, aliungana jukwaani na wasanii John Legend, DJ Khaled, Dr. Dre na Snoop Dogg, jambo linaloongeza matarajio kuhusu burudani atakayoileta katika hafla hiyo.




