Tanzania yashika nafasi ya tatu kuogelea Afrika

KAMPALA: TIMU ya Taifa ya Kuogelea Tanzania imeshika nafasi ya tatu katika matokeo ya jumla ya Mashindano ya Kuogelea ya Kanda ya Tatu Afrika yaliyofanyika nchini Uganda, baada ya kutwaa jumla ya medali 85.
Timu hiyo iliyokuwa na wanamichezo 35, imetwaa medali 24 za dhahabu, 29 za fedha na 32 za shaba, pamoja na vikombe nane.
Katika mashindano ya kuogelea kwenye maji ya wazi (Open Water), Tanzania pia imeshika nafasi ya tatu, ikiendeleza mafanikio yake katika mashindano hayo ya kikanda.
Kwa upande wa mchezo wa *Water Polo*, timu ya vijana wadogo ya Tanzania nayo imefanya vizuri kwa kushika nafasi ya tatu na kutwaa kikombe cha mshindi wa tatu.
Mashindano hayo yalifanyika mwishoni mwa wiki ambapo Tanzania iliwakilishwa na zaidi ya vijana 30 katika mitindo tofauti.




