Ligi Kuu

Dladla: Yanga inadaiwa magoli, soka zuri

DAR ES SALAAM: KOCHA Msaidizi wa Yanga, Simon Dladla, amesema timu hiyo inadaiwa magoli, soka zuri na ushindani wa kiwango cha juu na mashabiki wake, akiahidi kupambana kuhakikisha inarejesha furaha kwa Wananchi kupitia matokeo mazuri.

Dladla amesema hayo Dar es Salaam leo akieleza kuwa Yanga imezitambua kasoro zilizoonekana katika mchezo uliopita na inaendelea kuzifanyia kazi ili kufanya vizuri katika mechi zinazofuata.

Amesema wanatambua kuwa matokeo ya mchezo uliopita yaliwakatisha tamaa mashabiki, lakini amesisitiza kuwa timu imejipanga kurekebisha makosa na kuonesha mwitikio unaotarajiwa ndani ya uwanja.

“Kwa Wananchi, tunafahamu kuwa tuliwakatisha tamaa katika mchezo uliopita kwa sababu hatukupata matokeo tuliyokuwa tunayatarajia. Tumeyatambua mapungufu yetu na tutafanya kazi kwa bidii. Tunafahamu kuwa tuna deni kubwa kwenu. Tunadaiwa magoli, tunadaiwa soka zuri na kiwango cha juu cha ushindani kila tunaposhuka uwanjani,” amesema Dladla.

Amesema kucheza nyumbani kunaiweka Yanga katika nafasi ya kupambana kwa nguvu, huku akisisitiza umuhimu wa wachezaji kufanya maamuzi ya haraka na sahihi wanapofika eneo la lango la wapinzani.

Kuhusu mabadiliko ya mfumo na mbinu, Dladla amesema yatategemea wachezaji watakaokuwapo, akieleza kuwa jukumu la kutekeleza mipango ya benchi la ufundi litakuwa mikononi mwao watakapokuwa uwanjani.

Ameongeza kuwa lengo kubwa la Yanga ni kurejea kwenye kiwango kinachotakiwa na kuhakikisha klabu hiyo inaendelea kupigania nafasi ya juu.

Dladla amewaomba mashabiki wa Yanga kuwa na subira, kuendelea kuiamini timu na kujitokeza kwa wingi uwanjani kutoa sapoti, akiahidi kuwa wachezaji na viongozi wataendelea kufanya kazi ili kuwapa matokeo yatakayowarejeshea tabasamu.

Baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo uliopita dhidi ya TRA kesho itashuka dimbani kuivaa Mashujaa kwenye Uwanja wa KMC ikiwa chini ya Kocha huyo Msaidizi baada ya aliyekuwepo kutimuliwa.

Related Articles

Back to top button