Warembo 15 kutikisa Miss Kinondoni Oktoba 25 Serena

DAR ES SALAAM: WAREMBO 15 kuwania taji la Miss Kinondoni 2026, katika fainali inayotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu, katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Warembo hao wapo kambini kwa ajili ya maandalizi maalumu, yakuwajengea uwezo na kuwanoa katika nyanja mbalimbali za mashindano ya urembo kabla ya kuwania taji hilo.
Akizungumzia maandalizi ya mashindano hayo, Mkurugenzi wa Kampuni ya SPM Entertainment na Miss Kinondoni 2026, Salome Kikwembe, amesema maandalizi yanaendelea vizuri huku wakijipanga kuhakikisha mashindano ya mwaka huu yanakuwa na ushindani mkubwa.
Kikwembe amesema moja ya malengo yao ni kuandaa mshiriki atakayekuwa na uwezo wa kufanya vizuri katika mashindano ya Miss Tanzania na hatimaye kutwaa taji hilo la taifa.
Amefafanua kuwa warembo hao wapo kambini kujifua na kujiandaa kikamilifu, huku akiahidi kuwa fainali ya mwaka huu itapambwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali.
“Tumeshanza maandalizi ambapo warembo wapo kambini kujinoa kwa mashindano. Fainali ya mwaka huu itakuwa ya aina yake.
“Tunajivunia warembo wenye sifa ambao wana uwezo wa kupambana na kutwaa taji la Miss Tanzania,” amesema Kikwembe.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuwa fursa kwa warembo hao kuonyesha vipaji, uwezo na kujiamini, huku wadau wa urembo wakisubiri kuona atakayefanikiwa kutwaa taji la Miss Kinondoni 2026 na kuwania nafasi ya kuiwakilisha Kinondoni katika hatua zinazofuata za mashindano ya urembo nchini.




