Mitindo

Warembo 13 kuwania taji la Miss Ilala 2026

DAR ES SALAAM: WAREMBO 13 wanatarajiwa kushindana katika fainali za Miss Ilala 2026, zitakazofanyika Oktoba 24, mwaka huu, katika Ukumbi wa The Dreamer’s Lounge, Chanika, Dar es Salaam, huku washindi watano wa kwanza wakitarajiwa kupata nafasi ya kuiwakilisha wilaya hiyo katika shindano la Miss Tanzania 2026.

Uzinduzi wa shindano hilo ulifanyika jana katika Ukumbi wa Hoteli ya Nemart, Pugu Kinyamwezi, Dar es Salaam, ambapo waandaaji walieleza kuwa maandalizi yamekamilika kwa kiasi kikubwa na washiriki tayari wameingia kambini kujiandaa na fainali.

Akizungumza na Spoti leo katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Shindano la Miss Tanzania 2026, Diana Rutainurwa, amesema wamejipanga kuhakikisha msimu huu wa Miss Ilala unakuwa wa kipekee na kufanyika kwa ufanisi mkubwa.

Diana amesema warembo wote 13 wanaoshiriki shindano hilo wana sifa zinazohitajika, huku akieleza kuwa wana matumaini washindi watano wa kwanza wataiwakilisha Ilala vizuri katika shindano la Miss Tanzania mwaka huu.

“Tumefanya uzinduzi huu kuashiria kwamba maandalizi ya shindano yamekamilika na tupo tayari kwa fainali za Miss Ilala 2026.

Warembo 13 wanatarajia kushiriki, na tayari wapo kambini kufanya maandalizi ya mwisho,” amesema Diana.

Ameongeza kuwa fainali hizo zitapambwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali, hatua inayotarajiwa kuongeza mvuto kwa mashabiki na wadau watakaohudhuria tukio hilo.

Amesema wanaamini kuwa warembo watakaopatikana katika nafasi tano za juu watakuwa na uwezo wa kushindana na warembo wengine kutoka maeneo mbalimbali nchini katika kinyang’anyiro cha Miss Tanzania 2026.

Aidha, Diana ameomba ushirikiano na sapoti kutoka kwa viongozi wa Wilaya ya Ilala pamoja na wadau mbalimbali ili kuhakikisha shindano hilo linafanyika kwa mafanikio na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

“Tunaomba sapoti ya kutosha kutoka kwa viongozi wa Wilaya ya Ilala na wadau mbalimbali ili kuhakikisha shindano linafanyika kwa ufanisi na kufikia malengo yetu,” amesema.

Amefafanua kuwa kabla ya fainali kutakuwa na shindano la awali litakalotumika kuwapata washindi katika vipengele mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya shughuli zitakazoambatana na maandalizi ya fainali za Miss Ilala 2026.

Related Articles

Back to top button