La Liga

Real Madrid yamtaka Rais wa La Liga Javier Tebas jiuzulu

MADRID: TIMU ya Real Madrid imewataka rais wa La Liga, Javier Tebas, kujiuzulu kufuatia kauli yake iliyolinganisha juhudi za klabu hiyo za kuwashutumu waamuzi na mbinu za propaganda zilizotumiwa na Joseph Goebbels, aliyekuwa mkuu wa propaganda wa utawala wa Nazi nchini Ujerumani.

Tebas alitoa kauli hiyo Ijumaa kupitia mtandao wa kijamii wa X, akidai kuwa televisheni rasmi ya Real Madrid mara kwa mara huashiria kuwa waamuzi wanajaribu kuizuia klabu hiyo kupata ushindi katika mechi zake.

Rais huyo wa La Liga alisema mbinu hizo zinakumbusha mifumo ya propaganda iliyotumiwa na Goebbels, aliyekuwa mmoja wa viongozi muhimu wa utawala wa Adolf Hitler.

Kauli hiyo imeibua mvutano kati ya uongozi wa La Liga na Real Madrid, huku klabu hiyo ikichukua msimamo mkali dhidi ya matamshi ya Tebas na kutaka aondoke kwenye nafasi yake ya uongozi.

Real Madrid imekuwa ikitumia televisheni yake kuchambua maamuzi ya waamuzi katika michezo mbalimbali, jambo ambalo limekuwa likizua mijadala kuhusu usimamizi wa waamuzi na uadilifu katika soka la Hispania.

Kwa upande wake, Tebas amekuwa akijulikana kwa kauli zake za wazi kuhusu masuala yanayohusu soka la Hispania na mara kadhaa ameingia katika mabishano na viongozi wa klabu mbalimbali.

Mvutano huu unaongeza mgogoro kati ya Real Madrid na uongozi wa La Liga, huku kauli zilizotolewa zikitarajiwa kuendelea kuzua mjadala kuhusu uhuru wa kutoa maoni, ukosoaji wa waamuzi na wajibu wa viongozi wa soka.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button