ZIFF kupeleka filamu mikoa mitano Bara

DAR ES SALAAM: TAMASHA la Kimataifa la Filamu Zanzibar (ZIFF), kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) na nchi wanachama wake, limeandaa maonesho ya filamu katika mikoa mitano ya Tanzania Bara kwa lengo la kuimarisha ubadilishanaji wa kitamaduni na kuwapa vijana fursa ya kujifunza kupitia sanaa na teknolojia.
Maonesho hayo kupitia mradi wa ZIFF Goes Mainland 2026 yanatarajiwa kuanza kesho, Oktoba 20, katika kituo cha Alliance Française jijini Dar es Salaam, yakifuatiwa na shughuli nyingine Bagamoyo, Iringa, Mwanza na Dodoma hadi Desemba 2.
Mtendaji Mkuu wa ZIFF, Joseph Mwale, amesema ushirikiano kati ya taasisi hiyo na Umoja wa Ulaya umedumu kwa miaka mingi, huku mradi wa kupeleka filamu Tanzania Bara ukiwa umefikia toleo la tano mwaka huu.
Amesema filamu zitakazooneshwa zitatoka katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na Tanzania, zikigusa masuala mbalimbali ikiwemo akili unde (AI), mabadiliko ya tabianchi na uhusiano wa binadamu na teknolojia.
Mwale amesema maonesho hayo yatafanyika zaidi katika vyuo vikuu ili kuwafikia vijana na kuwapa nafasi ya kutazama filamu, kujadiliana na kujifunza kuhusu fursa za masomo na kubadilishana uzoefu, zikiwemo programu za Erasmus.
Kwa upande wake, Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Jean Marc Pisani amesema filamu ni nyenzo muhimu ya kuunganisha watu wenye tamaduni tofauti, kujenga uelewano na kufungua mijadala kuhusu changamoto zinazoikabili dunia.
Ameongeza kuwa tasnia ya filamu inaweza pia kutengeneza ajira kwa vijana katika maeneo kama uzalishaji wa filamu, ufundi na ujasiriamali wa kidijitali.
Filamu ya A Land apart ya Nigeria, iliyoshinda tuzo ya filamu bora katika ZIFF 2026, ndiyo itakayofungua maonesho hayo jijini Dar es Salaam.
Programu hiyo itashirikisha filamu kutoka nchi 10 za Umoja wa Ulaya, zikiwemo Ufaransa, Finland, Denmark, Ujerumani, Hispania, Italia, Sweden, Ireland na Poland.




