Reggie McFadden afariki akiwa Tanzania

NEW YORK: MKONGWE Reggea McFadden, anayefahamika zaidi kama mchekeshaji katika vipindi vya Def Comedy Jam vya HBO na In Living Color vya Fox, amefariki dunia akiwa na miaka 57.
Dada wa Reggie, mwandishi Bernice McFadden, ameuambia Mtandao wa TMZ kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliwasiliana na familia yao jana Jumapili na kuwapa taarifa hiyo.
Amesema wizara imewaeleza Reggie amefariki nchini Tanzania, alikokuwa akiishi kwa takriban miaka 18, lakini haikusema alifariki lini au kwa namna gani.
Bernice amefunguka, mwigizaji huyo kwa muda mrefu alikuwa ametengana na familia yake kutokana na masuala ya ndani ya kifamilia.
Aidha, Reggie pia aliwahi kung’ara kwenye vipindi vya ucheshi kama Martin, Hanging With Mr. Cooper, Moesha na Coach.
Baadhi ya vyanzo vinaeleza, Reggie alipotua Tanzania alijishughulisha na muziki pamoja na shughuli za ubunifu.
Alimiliki kampuni ya Olduvai Records, ilijiyojihusisha na uchimbaji wa dhahabu pamoja na uzalishaji wa kazi za burudani, huku usambazaji wake ukifanywa kupitia The Orchard ya Sony Music.
Imeripotiwa kuwa chini ya lebo hiyo, alitoa albamu yake ya Enjoy Vol. 1 mnamo Mei, mwaka jana.




