Filamu

Ben Affleck akanusha kuunganishwa kimapenzi na Shakira

LOS ANGELES: MUIGIZAJI na mkurugenzi wa filamu, Ben Affleck, amekanusha taarifa kwamba alijaribiwa kuunganishwa kimapenzi na mwimbaji Shakira baada ya kuvunjika kwa ndoa yake na Jennifer Lopez.

Affleck, mwenye umri wa miaka 54, amesema kwa sasa suala la mahusiano ya kimapenzi si kipaumbele kikubwa katika maisha yake, akieleza kuwa muda wake mwingi unatumika katika kazi na kuwa pamoja na watoto wake.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa filamu yake ‘Animals’ mjini Los Angeles, Affleck alisema maisha yake kwa sasa yamejikita zaidi katika kazi na familia.

“Ninafanya kazi sana, na ninatumia muda na watoto wangu. Hakuna nafasi kubwa ya kufanya mambo mengine nje ya hayo na kazi yangu. Sizunguki huku na kule,” amesema Affleck.

Affleck pia alikanusha taarifa zilizotolewa hivi karibuni na mtangazaji wa kipindi cha The View, Ana Navarro, kwamba aliwahi kujaribu kumtambulisha Affleck kwa Shakira baada ya kutengana na Lopez.

Navarro alidai kuwa alijaribu kuwaunganisha wawili hao, licha ya kukiri kwamba hajawahi kukutana na Affleck. Akijibu madai hayo, Affleck alisema hakuwahi kusikia kuhusu mpango huo.

“Kwa kweli, nasikia mambo kama hayo kutoka kwa watu kama wewe. Naapa kwa Mungu, sijawahi kusikia jambo hilo katika maisha yangu yote,” amesema Affleck.

Affleck na Jennifer Lopez walifunga ndoa mwaka 2022, baada ya kurejea katika uhusiano wao uliokuwa umesitishwa miaka kadhaa kabla. Hata hivyo, uhusiano wao ulifikia kikomo na wawili hao wakaachana.

Kwa sasa, Affleck amesema hana haraka ya kuingia katika uhusiano mwingine, akisisitiza kuwa kazi na watoto wake vinaendelea kuwa sehemu kubwa ya maisha yake.

Related Articles

Back to top button