Mastaa

Steve Nyerere awachana wanaomrekodi mgonjwa Zahir Ally Zorro

DAR ES SALAAM: MSANII wa filamu nchini Steve amesema ni jambo jema kwa watu kumtembelea na kumfariji gwiji huyo wa muziki, lakini amesisitiza kuwa wanapaswa kuzingatia hali aliyonayo na kulinda heshima na faragha yake.

“Sio sawa, watu wanaenda pale kwa Mzee Zorro, hata kama unamletea riziki, lakini ndiyo upige naye video?” amehoji Steve.

Ameongeza kuwa kupiga picha na mgonjwa si jambo linalokatazwa, lakini kinachopaswa kuzingatiwa ni hali ya mgonjwa wakati huo.

“Kupiga picha na mgonjwa hakukatazwi, lakini mgonjwa yupo kwenye hali gani?” ameongeza.

Akizungumzia kauli hiyo, mtoto wa Zahir Ally Zorro, Banana Zorro, amesema maoni ya Steve Nyerere yamekuja wakati mwafaka, akieleza kuwa familia yao haifurahishwi na picha na video zinazosambazwa zikimuonesha baba yao katika hali yake ya sasa.

“Kwa kweli sisi kama familia zile picha hazitupendezi, ingawa Mzee wetu ni mkarimu, mcheshi na mpenzi wa kupiga picha, lakini kwa sasa si jambo sahihi,” amefafanua Banana Zorro.

Kauli hiyo inaweka msisitizo kuhusu umuhimu wa kuheshimu faragha na utu wa watu wanaokwenda kuwajulia hali, hususan wanapokuwa katika mazingira yanayohitaji uangalizi na faragha zaidi.

Familia na wadau wa muziki wanahimizwa kuendelea kumfariji Zorro, huku wakizingatia heshima yake na matakwa ya familia yake.

Related Articles

Back to top button