Fola amzawadia mama yake gari

LAGOS: Msanii chipukizi wa muziki wa Nigeria, Folarin Odunlami, maarufu Fola, amezua gumzo baada ya kumshangaza mama yake kwa zawadi ya gari aina ya Lexus, katika tukio lililogusa hisia za mashabiki wake.
FOLA, ambaye amekuwa akipata umaarufu mkubwa katika muziki wa Afrobeats, ameamua kumuenzi mama yake kwa zawadi hiyo ikiwa ni sehemu ya kumshukuru kwa mchango na malezi yake.
Mbali na zawadi hiyo, msanii huyo pia ameelezwa kutimiza moja ya ndoto za muda mrefu za mama yake, inayohusiana na ujenzi wa kanisa, hatua iliyoongeza hisia na gumzo miongoni mwa mashabiki.
Tukio hilo limepokea maoni mbalimbali kutoka kwa mashabiki kwenye mitandao ya kijamii, huku wengi wakimpongeza FOLA kwa kumkumbuka na kumthamini mama yake wakati akiwa bado anaendelea kujenga jina lake katika tasnia ya muziki.
FOLA ni miongoni mwa wasanii wanaochipukia nchini Nigeria na amekuwa akivutia mashabiki kupitia muziki wake na ushirikiano na wasanii mbalimbali.




