Mr. Cheeks wa Lost Boyz kunogesha miaka 30 ya Bongo Fleva Arusha

ARUSHA: Msanii mkongwe wa Hip Hop kutoka Marekani, Mr. Cheeks, anatarajiwa kutua jijini Arusha Septemba 19 mwaka huu, kwa ajili ya kushiriki tamasha la kuadhimisha miaka 30 ya muziki wa Bongo Flava.
Mr. Cheeks, anayefahamika pia kama mmoja wa waanzilishi wa kundi maarufu la Hip Hop, Lost Boyz, anatarajiwa kuungana na mashabiki wa muziki katika tamasha hilo maalum litakalofanyika jijini Arusha.
Ujio wa msanii huyo unatarajiwa kuongeza mvuto katika tamasha hilo, huku mashabiki wakipata fursa ya kumuona na kumsikiliza moja kwa moja msanii huyo ambaye amekuwa sehemu ya historia ya Hip Hop duniani.
Tamasha hilo linatarajiwa kuwakutanisha wasanii pamoja na wadau mbalimbali wa muziki, katika kusherehekea safari ya miaka 30 ya Bongo Flava, muziki ambao umeendelea kukua na kupata umaarufu ndani na nje ya Tanzania.
Taarifa za ujio wa Mr. Cheeks NI matukio makubwa ya burudani jijini Arusha Kwa mwezi Septemba.
Kwa mashabiki wa Hip Hop wa kizazi cha zamani, ujio wa Mr. Cheeks unatajwa kuwa fursa ya kipekee ya kushuhudia moja kwa moja msanii huyo aliyewahi kutamba kupitia kundi la Lost Boyz.




