EPL

Newcastle yamsajili Dedi kwa Pauni 30 milioni

LONDON: NEWCASTLE United imekamilisha usajili wa beki Amar Dedi kutoka Benfica ya Ureno kwa ada inayokadiriwa kufikia Pauni milioni 30, huku mchezaji huyo akitia saini mkataba wa miaka mitano.

Dedi, ambaye ametimiza miaka 24 leo, Jumanne, Agosti 18, alifanyiwa vipimo vya afya Newcastle Jumatatu kabla ya kukamilisha uhamisho huo.

Usajili huo unamrejesha Dedi kufanya kazi na kocha Matthias Jaissle, ambaye aliwahi kumfundisha wakati wakiwa Red Bull Salzburg na kusaidiana kutwaa ubingwa wa Austria mwaka 2023.

Akizungumza baada ya kutangazwa kwa usajili huo, Dedi amesema ana furaha kubwa kujiunga na Newcastle na kusubiri kwa hamu kuanza kucheza mbele ya mashabiki wa klabu hiyo.

“Ni hisia za kipekee na heshima kubwa kwangu kujiunga na Newcastle. Nina furaha sana kuwa hapa na siwezi kusubiri kuanza kucheza kwa ajili ya klabu na mashabiki wake,” amesema Dedi.

Dedi amejiunga na Newcastle baada ya klabu hiyo kuhitaji beki wa kulia kufuatia kuondoka kwa Kieran Trippier, aliyejiunga na Wolves kwa uhamisho wa bure baada ya mkataba wake kumalizika mwishoni mwa msimu uliopita.

Kocha Jaissle amesema anafurahia kurejea kufanya kazi na Dedi, akimtaja kuwa mchezaji mwenye uwezo wa kusaidia timu katika majukumu ya ulinzi na mashambulizi.

Dedi pia ana uzoefu wa kucheza katika Uwanja wa St James’ Park, ambapo msimu uliopita alikuwa sehemu ya kikosi cha Benfica kilichofungwa mabao 3-0 na Newcastle katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Hata hivyo, beki huyo hajawahi kucheza Ligi Kuu England na sasa atalazimika kuzoea kasi na ushindani wa ligi hiyo.

Newcastle inatarajia kumtumia Dedi katika mchezo wa kwanza wa msimu dhidi ya Liverpool Jumapili, huku Tino Livramento akiwa bado anauguza majeraha ya misuli aliyoyapata akiwa kwenye majukumu ya timu ya taifa ya England.

Dedi ni miongoni mwa wachezaji sita waliosajiliwa na Newcastle katika dirisha hili la usajili, huku klabu hiyo ikiendelea kutafuta nyongeza nyingine kabla ya dirisha kufungwa Septemba 1.

Related Articles

Back to top button