Mwana FA: Burudani haijaishia, karibuni Kizimkazi festival ni moto

DAR ES SALAAM: NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’, amewakaribisha Watanzania na wageni mbalimbali kuhudhuria Tamasha la Kizimkazi Festival, akisema burudani haijaishia kwenye Dabi ya Kariakoo iliyofanyika inaendelea.
Mwinjuma amesema hayo muda mfupi baada ya kumalizika kwa mchezo huo, akieleza kuwa leo ndiyo kilele cha Tamasha la Kizimkazi Festival, ambalo linatarajiwa kuwakutanisha wasanii mbalimbali kwa ajili ya kutoa burudani kwa mashabiki.
Kwa mujibu wa Mwinjuma, Dabi ya Kariakoo imewapa mashabiki burudani kupitia mchezo mzuri uliochezwa, lakini baada ya soka kumalizika, Watanzania wanaalikwa kuendelea na burudani katika Tamasha la Kizimkazi Festival.
“Dabi ya Kariakoo imetupa burudani nzuri kupitia mchezo mzuri, lakini burudani haijaishia hapo. Leo tunahamia Kizimkazi Festival, ambapo wasanii mbalimbali watatoa burudani,” amesema Mwinjuma.
Ameongeza kuwa tamasha hilo linatarajiwa kuwa sehemu nyingine ya kuwapa Watanzania na wageni burudani, huku wasanii mbalimbali wakitarajiwa kutumbuiza katika kilele cha tamasha hilo.
Mwinjuma amesisitiza kuwa Watanzania wajitokeze kwa wingi kushiriki tamasha hilo na kuendelea kufurahia burudani zinazotolewa na wasanii wa Tanzania.




