TID kutumbuiza tamasha la miaka 30 ya bongo fleva

DODOMA: Msanii mkongwe wa Bongo Fleva, Khalid Mohamed ‘TID’, ameomba radhi kwa wasanii wenzake, waandaaji na mashabiki baada ya kauli yake ya awali kuhusu Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Fleva kuzua mjadala mkubwa mitandaoni.
TID, ambaye awali amesema Tamasha hilo kwake lilikuwa “dili ndogo sana”, sasa amebadili msimamo na kuweka wazi kuwa yuko tayari kushiriki katika Tamasha hilo litakapofanyika jijini Dodoma, endapo Waandaaji watampa nafasi.
Awali, TID alisema mmoja wa waandaaji wa Tamasha hilo, Madee, alimpigia simu na kumuomba kushiriki katika uzinduzi pamoja na maandalizi ya Tamasha hilo.
Hata hivyo, msanii huyo alikataa kutokana na kuwa na mkataba mwingine wa kibiashara alioueleza kuwa ulikuwa na maslahi makubwa kwake.
Kauli hiyo ilizua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, huku baadhi ya Mashabiki na wadau wa muziki wakimkosoa, wakati wengine wakitetea uamuzi wake wa kuzingatia maslahi ya mkataba aliokuwa nao.
Katika hatua mpya, TID kupitia video ameomba radhi kwa Wasanii wenzake, Waandaaji na Mashabiki kutokana na kauli yake ya awali.
Msanii huyo amesema amesikiliza maoni ya Mashabiki wake na sasa yuko tayari rasmi kurejea kwenye Tamasha hilo na kutumbuiza mbele ya Mashabiki wa Bongo Fleva.
TID amesema anachosubiri ni Waandaaji kumpa nafasi nyingine ya kushiriki katika Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Fleva litakapofika Dodoma.
Hatua hiyo imekuja wakati maandalizi ya maadhimisho ya miaka 30 ya Bongo Fleva yakiendelea, huku tamasha hilo likitarajiwa kuwakutanisha wasanii wakongwe na kizazi kipya katika kusherehekea safari ya burudani ya muziki.




