Ronaldo, Georgina wafunga ndoa

CASCAIS: NYOTA wa soka wa Ureno, Cristiano Ronaldo, 41, na mpenzi wake wa muda mrefu, Georgina Rodríguez, 32, wamefunga ndoa baada ya miaka nane ya safari ya mapenzi iliyowafanya kuwa moja ya familia zinazofuatiliwa zaidi duniani.
Ronaldo na Georgina walifunga ndoa katika sherehe binafsi iliyofanyika Cascais, Ureno, Agosti 11, 2026, huku watoto wao watano wakiripotiwa kuwepo katika tukio hilo.
Wawili hao walithibitisha ndoa yao kupitia mitandao ya kijamii kwa picha ikionesha mikono yao ikiwa imevalishwa pete za ndoa, huku Ronaldo akiambatanisha ujumbe mfupi wa “C❤️G”, uliowafanya mashabiki wao duniani kote kusherehekea hatua hiyo.
Ndoa hiyo imekuja mwaka mmoja baada ya Georgina kutangaza uchumba wao Agosti 2025, alipowaonesha mashabiki pete yake kubwa yenye umbo la mviringo na kusema atakubali kuwa mke wa Ronaldo.
Safari yao ilianza mwaka 2016, wakati Georgina alipokuwa akifanya kazi kama mhudumu wa mauzo katika duka la Gucci mjini Madrid, Hispania. Uhusiano wao ulizidi kukua na mwaka 2017 wakaanza kuonekana hadharani pamoja katika hafla kubwa za soka.
Katika kipindi hicho, wawili hao wamejenga familia yenye watoto watano, akiwamo Cristiano Jr, mapacha Eva Maria na Mateo, Alana na Bella.
Hata hivyo, safari yao haikuwa ya furaha pekee. Mwaka 2022 walipitia kipindi kigumu baada ya kutangazwa kwa kifo cha mtoto wao wa kiume, Ángel, pacha wa Bella, muda mfupi baada ya kuzaliwa.
Tukio hilo liliwaweka kwenye wakati mgumu, lakini waliendelea kusimama pamoja na kujenga familia yao huku Ronaldo akiendelea na maisha yake ya soka katika kiwango cha juu.




