Picha za Zari, Shakib zazua minong’ono mtandaoni

KAMPALA: Baada ya kutangaza kuachana mwezi uliopita kutokana na kile walichokiita tofauti zisizoweza kusuluhishwa, mastaa wa Afrika Mashariki Zari Hassan maarufu kama Zari The Boss Lady na mumewe Shakib Cham wamezua gumzo jipya kufuatia kusambaa kwa picha mpya zinazowaonesha wakiwa pamoja kwa ukaribu nchini Uganda.
Picha hizo, ambazo zimesambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii, zimewaonesha wawili hao wakionekana wenye furaha na ukaribu mkubwa, hali iliyowafanya mashabiki wengi kuanza kuhoji kama wameamua kumaliza tofauti zao na kuurudisha rasmi uhusiano wao.
Wengine wameeleza kuwa huenda walikuwa kwenye mapumziko ya pamoja, huku wengine wakisubiri uthibitisho rasmi kutoka kwa wawili hao.
Hadi sasa, Zari na Shakib hawajatoa tamko rasmi kuthibitisha kuwa wamerudiana, jambo linaloacha nafasi kwa uvumi kuendelea kutawala mitandaoni. Hata hivyo, picha hizo zimeendelea kuchochea mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki wao Afrika Mashariki na kwingineko.
Zari na Shakib walitangaza kuachana mwezi Juni 2026 kupitia taarifa ya pamoja wakieleza kuwa wamefikia uamuzi huo baada ya kutafakari kwa kina, huku wakisisitiza kuwa waliendelea kuheshimiana licha ya kuvunjika kwa ndoa yao.
Kuonekana kwao pamoja kwa mara nyingine sasa kumefufua matumaini ya mashabiki wanaotamani kuwaona wakirekebisha tofauti zao.




