Tonny Rashid kumvaa Juma Choki Dar Boxing Debi

DAR ES SALAAM: BONDIA Tonny Rashid amerejea nchini akitokea Afrika Kusini baada ya kukamilisha kambi ya maandalizi kuelekea pambano lake dhidi ya Juma Choki litakalofanyika Julai 24, 2026 katika tamasha la Dar Boxing Debi jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Rashid amesema maandalizi yake yamekwenda vizuri na sasa amerejea kukamilisha programu za mwisho nchini kabla ya kupanda ulingoni.
Bondia huyo amesema ana imani kubwa ya kuibuka na ushindi kutokana na mazoezi aliyoyafanya nchini Afrika Kusini, huku akiwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kushuhudia pambano hilo.
Kwa upande wake, kocha wake Amos Nkondo, maarufu kama Kocha Amoma, amesema kila kitu kinaendelea vizuri na kikosi chao kipo tayari kwa pambano hilo.
Amesisitiza kuwa wamejiandaa vya kutosha na kuwaahidi Watanzania pamoja na mashabiki wa bondia huyo kuwa wataondoka na ushindi siku ya pambano.




