Waamuzi Tanzania kuichezesha Kenya, Sudan Kusini

WAAMUZI wanne wa Tanzania, Florentina Zablon, Janeth Balama, Helen Mduma na Jonesia Rukyaa wameteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuchezesha mchezo wa kufuzu Mataifa ya Afrika (Afcon) kwa wanawake kati ya Kenya na Sudan Kusini.
Mchezo huo utakaozikutanisha timu kutoka ukanda wa Afrika Mashariki, utafanyika Oktoba 23 katika Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi, Kenya.
Akizungumzia kuwa mwamuzi wa mchezo huo jana, Zablon alisema hiyo ni heshima kwao kwa kupata nafasi hiyo, hivyo wanajipanga kwenda kufanya vizuri kwa kuchezesha kwa haki, huku wakifuata sheria zote za mpira wa miguu.
“Ni heshima kwetu kupata nafasi hii tunaenda nchini Kenya kufanya kazi kama ambavyo tumekuwa tukifanya katika mashindano ya hapa nchini.”
“Hii haitakuwa mara yetu ya kwanza kuchezesha mashindano makubwa ya nje ya nchi, tunaenda tukiwa na matumaini ya kufanya vizuri na kurejesha heshima kwa nchi yetu,” alisema Zablon.