Miss Universe apingwa mitandaoni

THAILAND: Shindano la 74 la Miss Universe 2025 limetamatika nchini Thailand, na mrembo wa Mexico, Fatima Bosch, ametangazwa mshindi wa taji la dunia. Hata hivyo, mtandaoni kumekuwa na hisia mseto, baadhi wakipongeza ushindi wake huku wengine wakipinga matokeo hayo.
Wengi waliodhani kuwa mwakilishi wa India Manika Vishwakarma ambaye ni mwanafunzi wa sayansi ya siasa mwenye miaka 21, hakufanikiwa kuingia katika orodha ya Warembo 12 Bora, jambo lililowashangaza wengi.
Licha ya mvuto na mvutano wa mavazi, tabasamu na utamaduni wa mataifa, shindano la mwaka huu lilitikiswa na mizozo zaidi kuliko miaka ya nyuma.
Hali ya sintofahamu ilianza baada ya madai ya kudhalilishwa kwa akili ya mmoja wa warembo, hali iliyochochea washiriki wengine kuchukua uamuzi mkali wa kuondoka jukwaani. Wakati huohuo, mtangazaji wa shindano hilo alishindwa kujizuia na kulia hadharani kutokana na presha ya tukio hilo kumzidi.
Mrembo wa Mexico, Fatima Bosch, ambaye sasa ndiye mwenye taji la Miss Universe 2025, alishangaza mashabiki kwa kuondoka ghafla kwenye mkutano akiwa bado na gauni lake la usiku huku akiwa amevalia viatu virefu baada ya kukemewa hadharani na mwenyeji wa shindano, Nawat Itsaragrisil.
Katika matangazo ya moja kwa moja, Nawat alionekana kumlenga Miss Mexico na kumdhihaki huku akimkosoa kwa madai kuwa hakushiriki ipasavyo maudhui ya matangazo kwenye mitandao yake ya kijamii. Tukio hilo liliibua mjadala mkali mtandaoni na kuacha mashabiki wakiwa na maswali kuhusu mwenendo wa shindano hilo.
Katika mazingira haya ya vurugu, hadi majaji watatu waliripotiwa kuondoka, mmoja wao akidai kuwepo kwa uhusiano wa kimapenzi kati ya mshiriki na jaji madai ambayo yameongeza utata mkubwa kuelekea uhalali wa matokeo ya mwaka huu.
Wakati Miss Universe 2025 ikiendelea kujadiliwa kwa hisia kali, imetangazwa rasmi kuwa Puerto Rico ndilo litakalokuwa mwenyeji wa shindano la mwaka 2026.



