Le Normand aumia goti, kukosa mechi kadhaa

MADRID: KLABU ya Atletico Madrid imethibitisha kuwa beki wake Robin Le Normand, amepata jeraha kubwa katika eneo la nyuma ya goti lake la kushoto wakati wa ushindi wao wa mabao 3-1 dhidi ya Union Saint-Gilloise (USG) kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya usiku wa Jumatano.
Nyota huyo wa kimataifa wa Hispania alilazimika kufanyiwa mabadiliko katikati ya kipindi cha kwanza katika mchezo huo uwanja wa nyumbani dhidi ya timu hiyo ya Ubelgiji, baada ya kugongana na mchezaji wa USG na kuonekana kuwa maumivu makali.

Taarifa za madaktari zinasema kuwa uchunguzi wa awali umeonesha kuwa jeraha hilo limetokana na kunyooshwa kupita kiasi kwa goti (hyperextension), na limeathiri mfupa wa nyuma (posterior capsule) pamoja na misuli ya semimembranosus, ingawa mifupa ya goti na meniskasi hazijaathirika.
Ripoti za vyombo vya habari nchini Hispania zinasema beki huyo mwenye umri wa miaka 28 huenda akakosa kucheza kwa takribani mwezi mmoja, hali itakayomfanya kuukosa mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia kati ya Hispania na Georgia tarehe 15 Novemba, pamoja na mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Inter Milan utakaochezwa Novemba 26.




