Mbappe mambo safi Azam FC

DAR ES SALAAM: BAADA ya kuwa nje ya uwanja kwa takribani miezi miwili akiuguza majeraha ya goti, kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Cheickna Diakite ‘Mbappe’ amerejea mazoezini na yuko tayari kuivaa Namungo.
Diakite, ambaye ni miongoni mwa wachezaji muhimu katika safu ya ushambuliaji ya “Wanalambalamba”, ameonekana akiwa na ari kubwa wakati akiungana na wenzake kwa mara ya kwanza tangu alipoumia mapema msimu huu.
Kurejea kwake kunakuja wakati muafaka, kikosi cha Azam FC kikiwa kimerejea kambini kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Namungo FC, utakaopigwa Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa, mkoani Lindi, siku ya Jumapili, saa 1.00 usiku.
Kurejea kwa Diakite kutaleta chachu mpya kwenye kikosi, hasa katika eneo la kati na mbele ambapo ubunifu wake na kasi vinatajwa kuwa silaha muhimu kwa timu hiyo inayopigania nafasi ya juu kwenye msimamo wa ligi.
Mchezaji huyo aliyejiunga na Azam FC mapema msimu huu akitokea AS Real ya Bamako Mali, bado ana kazi ya kuhakikisha anatafuta namba kwenye kikosi cha kwanza chini ya Kocha Mkuu Frorent Ibenge.



