Bundesliga

Dortmund yajijiamini kuelekea ‘der klassiker’ dhidi ya Bayern

DORTMUND: KOCHA wa Borussia Dortmund, Niko Kovac, amesema morali ya timu yake iko juu kufuatia mwenendo wao mzuri wa kutopoteza mechi yoyote msimu huu, wakielekea kwenye mchezo wa ‘Der Klassiker’ dhidi ya mahasimu wao mabingwa watetezi Bayern Munich kesho Jumamosi.

Dortmund, ambao wako nafasi ya pili kwenye msimamo wa Bundesliga wakiwa nyuma ya Bayern kwa pointi nne, hawajapoteza mchezo wowote kwenye Bundesliga wala ligi ligi ya mabingwa Ulaya tangu msimu huu uanze. Bayern kwa upande wao wameshinda michezo kumi mfululizo katika mashindano yote, na kuonesha ubora wa hali ya juu.

“Kikosi kiko imara kwa sasa, na huo ndio msingi wa mafanikio yoyote, Tunatambua ubora wa Bayern, kushinda mechi 10 kati ya 10 sio mchezo. Wana wastani wa alama tatu kwa mchezo, wakati sisi tuna wastani wa alama 2.3. Hiyo inaonesha ubora wao, lakini nasi tuko kwenye njia nzuri na tupo tayari kwa changamoto hii ngumu.” – Kovac alisema katika mkutano na waandishi wa habari mjini Dortmund.

 

Mchezo huo wa Jumamosi utakuwa wa kwanza kati ya mechi sita za ugenini kati ya saba zijazo za Dortmund katika mashindano yote, ikiwemo safari za mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenda Copenhagen wiki ijayo, na kisha Manchester City tarehe 5 Novemba.

Kovac amesema hawana mpango wa kucheza kwa tahadhari dhidi ya Bayern, akisisitiza umuhimu wa kuanza vizuri na kudhibiti mchezo mapema.

“Bayern mara nyingi hushinda michezo yao katika kipindi cha kwanza, kwa hiyo ni muhimu kuufanya mchezo ubaki wazi kwa muda mrefu iwezekanavyo. Tunapaswa kuanza kwa nguvu, kuwa na umoja na kuzuia wapinzani wasitutawale.”

“Ukicheza kwa uoga Munich ni vigumu kufanikiwa. Haiwezekani kwenda huko kujilinda tu, kwa sababu wanapachika wastani wa mabao manne kwa mchezo. Lakini nasi tuna ubora wetu katika safu ya ushambuliaji, na tunapaswa kuwapelekea presha.” – aliongeza

Mchezo huo unatarajiwa kupigwa kesho majira ya saa 1:30 saa za afrika mashariki kwenye uga wa Allianz arena jijini Munich

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button